Wahajiri 20 watiwa nguvuni wakiwa ndani ya malori huko Ubelgiji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56882-wahajiri_20_watiwa_nguvuni_wakiwa_ndani_ya_malori_huko_ubelgiji
Polisi ya Ubelgiji imetangaza kuwa, imekamata malori mawili yaliyokuwa yamebeba wahajiri 20 wakiwa njiani kupelekwa Uingereza.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 27, 2019 07:31 UTC
  • Wahajiri 20 watiwa nguvuni wakiwa ndani ya malori huko Ubelgiji

Polisi ya Ubelgiji imetangaza kuwa, imekamata malori mawili yaliyokuwa yamebeba wahajiri 20 wakiwa njiani kupelekwa Uingereza.

Taarifa ya Polisi ya Ubelgiji imesema kuwa, malori hayo mawili yalikamatwa jana yakiwa na wahajiri 20 katika eneo la Saint-Trond huko mashariki mwa mji wa Bruges kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Ripoti zinasema wahajiri 11 wanaojumuisha watoto na wanawake waliokuwa katika mojawapo ya magari hayo mawili ni Waafrika raia wa Eritrea. Polisi ya Ubelgiji inasema kuwa raia wengine 9 waliokuwa katika lori la pili ni wanaume kutoka Iraq.

Jumanne iliyopita pia polisi ya Ubelgiji iliwatia nguvuni watu watatu wenye asili ya Iraq wanaodhaniwa kuwa wafanyamagendo ya binadamu. Wafanyamagendo ya binadamu wanatumia ardhi ya Ubelgiji kama njia ya kusafirisha wahajiri haramu kuelekea Uingereza. 

Siku chache zilizopita polisi ya Uingereza iligundua maiti za wahajiri 39 zikiwa ndani ya lori lililokuwa limeegeshwa katika kitongoji cha Grey, eneo la Essex huko mashariki mwa London.

Lori lililokuwa na maiti za wahajiri, Uingereza

Dereva mwenye asili ya Ireland Kaskazini aliyekamatwa na polisi ya Uingereza akihusishwa na vifo hivyo anakabiliwa na tuhuma za mauaji bila ya kukusudia, magendo ya binadamu na kutakatisha fedha chafu. 

uchunguzi unaendelea ili kubaini utambulisho wa wahanga hao.