Malaysia: Marekani imetangaza vita kwa kumuua shahidi Soleimani
Baraza la Shura la Jumuiya ya Waislamu Malaysia limelaani vikali hatua ya kigaidi ya Marekani ya kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC.
Rais wa baraza hilo, Mohammad Azmi Abdul Hamid amesema katika taarifa kuwa, "Mauaji hayo ya Jenerali Soleimani yameionesha dunia kuwa Marekani ni taifa la kijambazi na lenye kupenda shari."
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, ni ubeberu na ubabe wa kupundikia kwa Marekani kujiona kama nchi yenye kibali cha kumuua yeyote inayemtaka.
Rais wa Baraza la Shura la Jumuiya ya Waislamu Malaysia ameeleza bayana katika taarifa hiyo kuwa, kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikitenda jinai ikifahamu kuwa dunia haiwezi kuiwajibisha, lakini amesisitiza kuwa mauaji ya Haji Soleimani hayatapita hivi hivi bila Washington kubebeshwa dhima na kuadhibiwa.

Ameongeza kuwa, jinai hiyo ya Marekani ni jambo lisilokubalika na kwamba hatua hiyo ya kigaidi haina tafsiri nyingine isipokuwa ni tangazo la wazi la vita.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Abu Mahdi al Muhandes, Naibu Kiongozi Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hashdu sh-Shaabi ya Iraq, pamoja na shakhsia wengine waliuawa shahidi asubuhi ya Ijumaa kupitia shambulio la kigaidi lililofanywa na kikosi cha anga cha Marekani katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Baghdad.