Uturuki yaanza kutuma vikosi vya jeshi lake nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58339-uturuki_yaanza_kutuma_vikosi_vya_jeshi_lake_nchini_libya
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimeanza kuelekea nchini Libya, kushirikiana na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 06, 2020 08:00 UTC
  • Uturuki yaanza kutuma vikosi vya jeshi lake nchini Libya

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimeanza kuelekea nchini Libya, kushirikiana na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj.

Erdogan alisema hayo jana Jumapili katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CCN ya Kituruki na kuongeza kuwa, "Kutakuwepo na kituo chetu cha operesheni nchini Libya kitakachosimamiwa na kuendeshwa na Luteni Jenerali wa Uturuki. Tayari askari wa Uturuki wameanza kuelekea nchini Libya hatua kwa hatua." 

Siku ya Alkhamisi, Bunge la Uturuki lilipasisha muswada wa sheria inayoruhusu kutumwa wanajeshi wa nchi hiyo huko Libya, licha ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuonya kuwa, "Hatua ya upande mmoja itakayopelekea kutumwa vikosi ajinabi nchini Libya haitakuwa na tija nyingine ghairi ya kushadidisha mgogoro unaolikumba taifa hilo."

Juzi Jumamosi, watu 30 kuuawa katika shambulizi la anga lililolenga chuo cha kijeshi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Inaaminika kuwa, wapiganaji wanaojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' ndio walitekeleza hujuma hiyo, ingawaje msemaji wa wanamgambo hao wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar amekanusha madai hayo.

Wanajeshi wa Uturuki

Wapiganaji wa Khalifa Haftar mwezi Aprili mwaka uliopita wa 2019 walianzisha mashambulizi ya kutaka kuudhibiti mji mkuu, Tripoli.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 2,000 wakiwemo raia 280 wameuawa jijini Tripoli na wengine wasiopungua 140,000 wamejeruhiwa tangu kuanza mashambulizi hayo ya kundi la wanamgambo wa Haftar, wanaoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani, Imarati na baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa.