Ghasia zashtadi India, waliouawa New Delhi wafika 24
Idadi ya waliouawa katika ghasia zilizosababishwa na sheria tatu yenye kuwabagua Waislamu katika mji mkuu wa India, New Delhi imeongezeka na kufikia watu 24.
Aidha mami ya watu wamejeruhiwa katika machafuko hayo ambayo leo Alkhamisi yanaingia siku yake ya nne huko kaskazini mashariki mwa Delhi, eneo ambalo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu.
Kadhalika misikiti kadhaa imevamiwa na kuteketezwa moto na makundi ya vijana wenye misimamo ya kibaguzi na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Watu walioshuhudia wanasema kuwa, askari polisi wa India waliwavamia waandamanaji na kutia mbaroni kadhaa miongoni mwao. Maandamano hayo yanafanywa na watu wanaounga mkono na wanaopinga sheria hiyo.

Ghasia hizi zinatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kuikumba India katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita, huku asasi za kijamii zikifanya pia maandamano ya amani ya kuitaka serikali iangalie upya sheria hiyo ya kibaguzi.
Sheria hiyo tata inaruhusu kupewa uraia wahajiri wasio Waislamu waliokimbilia India kutoka nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan, huku ukiwanyima haki hiyo ya uraia Waislamu.