Mar 01, 2020 02:39 UTC
  • Ugiriki yazuia kutolewa taarifa ya uungaji mkono wa NATO kwa Uturuki

Serikali ya Ugiriki imetumia haki yake ya turufu kuzuia kutolewa taarifa ya uungaji mkono wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kwa Uturuki.

Hatua hiyo ilitekelezwa tarehe 28 Februari na ujumbe wa uakilishi wa kudumu wa Ugiriki katika shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi. Kikao cha dharura cha NATO katika ngazi ya wawakilishi wa kudumu kiliitishwa kufuatia matukio ya kijeshi ya hivi karibuni yaliyojiri katika mkoa wa Idlib, Syria hususan baada ya kuuawa askari 33 wa Uturuki na kujeruhiwa wengine zaidi ya 30 kupitia shambulizi la anga. Nikos Dendias, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki alitoa amri kwa ujumbe wa kudumu wa nchi hiyo katika shirika hilo utumie haki yake ya turufu kupinga uungaji mkono huo iwapo taarifa ya pamoja ya Umoja wa Ulaya inayojumuisha mapendekezo ya serikali ya Athens kuhusiana na  ulazima wa kutekelezwa makubaliano ya Uturuki na Umoja wa Ulaya yaliyofikiwa mwezi Machi 2016 kuhusiana na wahajiri na wakimbizi, haitazingatiwa.

Uturuki na Ugiriki zimekuwa na mvutano wa siku nyingi

Pamoja na hayo takwa la Ugiriki lilikabiliwa na vikwazo vikali kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kama vile Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa. Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alikuwa ametaka kufanyike mazunguumzo ya kisiasa kuhusu kipengee cha nne cha mkataba wa NATO ambacho kinairuhusu nchi mwanachama kuomba msaada kwa shirika hilo la kijeshi iwapo nchi hiyo itabaini kwamba usalama, uhuru wa kisiasa na ardhi yake viko hatarini. Hakuna makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho ambapo kilimalizika bila kutolewa taarifa ya pamoja.

Tags