Mar 03, 2020 02:24 UTC
  • Polisi na raia wa Ugiriki wapambana na wahajiri wanaoingia Ulaya

Polisi na kundi la raia wa Ugiriki wamekabiliana na wahajiri wanaovuka mpaka kuelekea Ulaya.

Vurugu hizo zimetokea katika eneo la kisiwa cha Lesbos ambapo wakazi wa eneo hilo sambamba na kujaribu kuzuia kutia nanga boti moja ya wahajiri waliokuwa wanaelekea kisiwa hicho na kupiga nara zinazosema 'rudini Uturuki', wamevamia kambi moja ya wahajiri iliyo chini ya Umoja wa Mataifa na kuiteketeza kwa moto.

Vilevile polisi wa Ugiriki wamefyatua mabomu ya kutoa machozi katika mpaka wa nchi hiyo na Uturuki wakikabiliana na mamia ya wahajiri ambao walikuwa wanakusudia kuingia nchini humo. Serikali ya Athens imetangaza kwamba imeweza kuzuia karibu wahajiri elfu 10 kwenye mpaka wake na Uturuki na kuwahamishia katika kisiwa cha Évros.

Juhudi za kuzuia boti ya wahajiri kuingia Ugiriki

Viongozi wa Ugiriki wametangaza kwamba wamewatia nguvuni wahajiri 37 kutoka Afghanistan, Pakistan na Somalia. Shirika la Kimataifa la Wahajiri limetangaza kuwa, karibu wahajiri elfu 13 wamekusanyika kwenye mpaka wa Uturuki na Ugiriki.

Kufuatia kushtadi vita nchini Syria na kuongezeka uwezekano wa maelfu ya wahajiri kumiminika Ulaya, Ugiriki imechukua hatua kali za kuzuia wahajiri hao. Uturuki ambayo ni jirani na Ugiriki inawahifadhi wakimbizi milioni tatu wa Syria mkabala wa kupokea fedha kutoka kwa Umoja wa Ulaya.

Uturuki imekuwa ikitishia kwamba, itafungua mipaka yake ili kuwaruhusu wakimbizi hao kuingia Ulaya.

Tags