Kuthibitika kuwa uchumi wa Marekani umeingia katika mdororo mkubwa
Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitumai kutumia madai yake ya mafanikio ya kiuchumi katika kampeni zake za uchaguzi wa rais nchini humo mwaka huu wa 2020, lakini hakuwa ametabiri kuhusu kuenea ugonjwa wa COVID-19 au corona ambao umepelekea kuporomoka masoko ya hisa Marekani na hivyo kuingiza uchumi huo mkubwa zaidi duniani katika mdororo.
Kuhusiana na nukta hiyo, wataalamu wa uchumi katika benki ya Bank of America wameandika barua na kutahadharisha kuwa, uchumi wa Marekani sasa umeingia katika mdororo mkubwa. Michelle Meyer mchumi mwandamizi katika Bank of America ambayo ni benki ya pili kwa ukubwa Marekani, siku ya Alhamisi 19 Machi aliwaandikia barua wateja wa benki hiyo na kuwaonya kuwa, uchumi wa Marekani sasa umeingia katika mdororo mkubwa kutokana na janga la corona duniani.
Alisisitiza kuwa: "Tunatangaza rasmi kuwa, uchumi wa Marekani, sawa na uchumi wa nchi zingine duniani, umeingia katika mdororo ambao ni mkubwa na wa kina." Pamoja na hayo alidai kuwa mdororo huo ni wa muda mfupi.
Uchumi wa Marekani katika wiki za hivi karibuni umeathiriwa vibaya na janga la corona kiasi kwamba, katika mwezi huu wa Machi soko la hisa la New York limeporomoka kwa asilimia 30.
Huku janga la ugonjwa wa COVID-19 au corona likiendelea, kumeibuka wasiwasi mkubwa miongoni mwa wawekezaji Marekani. Moja ya nukta ambazo zimepelekea wawekezaji waingiwe na wasi wasi mkubwa ni majibu yasiyofaa ya serikali ya Trump kuhusu hali isiyo ya kawaida katika uchumi wa nchi hiyo. Aidha wana wasi wasi kuhusu kutojulikana hatima ya walioambukizwa corona nchini Marekani na kwamba hofu ya kuambukizwa corona imepelekea kuwekwa vizingiti vikubwa hasa kuwazuia watu kutoka nje na jambo hilo bila shaka litakuwa na taathira mbaya katika uuzaji bidhaa na yamkini likapelekea uchumi usambaratike.
Kwa kuzingatia hali hiyo kumewasilishwa utabiri hasi kuhusu uchumi wa Marekani. Kwa mfano benki ya Deutsche Bank ya Ujerumani imetabiri kuwa, thamani ya hisa katika masoko ya hisa ya Marekani itapungua kwa asilimia 15 hadi 20.
Tab'an Michelle Meyer, ambaye pia anahesabiwa kama mmoja wa wachumi wakubwa Marekani, anaamini kuwa, njia ya kukabiliana na kudorora uchumi nchini humo ni watekelezaji wa sera za fedha na uchumi kuanzisha mchakato maalumu wa vichocheo vya kibajeti na kifedha vya kukuza uchumi na kwamba vichocheo hivyo visiwe na mipaka.
Huu ndio mkakati ambao sasa umeanzishwa na Benki Kuu ya Marekani ambayo inajulikana kama Federal Reserve. Katika kukabiliana na athari hasi za corona katika uchumi, Federal Reserve ilitangaza Jumapili 15 Machi kuwa riba itapunguzwa kwa asilimia moja. Aidha benki hiyo imesema itamimina dola bilioni 700 katika soko nchini humo.
Pamoja na hayo, hatua hizo hazijaweza kuzuia uchumi wa Marekani kudorora na kuingia katika kinamasi. Hivi sasa idadi ya watu wasio na kazi imeongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu. Hii ni katika hali ambayo kwa muda mrefu Trump amekuwa akidai kuwa sera zake zimechangia kupungua ukosefu wa ajira nchini humo.
Waziri wa Fedha wa Marekani Steven Mnuchin amekiri kuwa yamkini kuibuka ugonjwa wa corona kukasababisha kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kufika asilimia 20. Amesema kuwa katika wmezi wa Februari pekee, kiwango cha ukosefu wa ajira kilifika asilimia 3.5. Weledi wa mambo wanasema taathira hasi za corona kwa uchumi zitakuwa mbaya zaidi ya ule mdororo wa kiuchumi wa mwaka 2008.
Kwa mujibu wa utabiri wa Jeffrey Tucker, mtaalamu mwandamizi wa masuala ya uchumi, "kuna uwezekano mkubwa kuwa Pato Ghafi la Taifa (GDP) Marekani likapata pigo kubwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2020 na hivyo kuwa na taathira katika kiwango cha ukosefu wa ajira.
Trump amekuwa akinadi mafanikio yake ya kiuchumi na kuyaona kuwa msingi mkubwa katika kumuwezesha kupata ushindi katika uchaguzi wa rais Novemba 2020. Lakini hali ya sasa ambayo haikutabiriwa imepelekea kuporomoka kwa kasi masoko ya hisa ya Marekani sambaba na ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira. Aidha uchumi wa Marekani sasa umechukua mkondo wa kudorora na hivyo hali ya kiuchumi nchini humo itazidi kuwa mbaya na Wamarekani wataendelea kuchukizwa na utendaji wa utawala wa Trump na kwa msingi huo uwezekano wake wa kupata ushindi katika uchaguzi unaendelea kudidimia.