Uchunguzi mpya wa maoni Marekani: Wagombea urais wa Democrat watambwaga Trump
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanyika nchini Marekani yanaonyesha kuwa ikiwa uchaguzi wa rais wa Marekani utafanyika hivi sasa, wagombea wa chama cha Democrat watamshinda rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump katika kinyang'anyiro hicho.
Tovuti ya taasisi ya uchunguzi wa maoni ya The Hill imeripoti kuwa uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti la kila wiki la Economist kwa kushirikiana na taasisi ya YouGov unaonyesha kuwa, asilimia 48 ya watu waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi ujao wa rais wa Marekani wamesema, katika kinyang'anyiro cha mwisho baina ya makamu wa zamani wa rais Joe Biden na Trump, watampigia kura Biden.
Aidha asilimia 48 ya wapiga kura wametangaza kuwa, endapo mchuano wa mwisho katika uchaguzi wa rais utakuwa baina ya Bernie Sanders na Trump, watampigia kura pia seneta huyo wa jimbo la Vermont.
Katika uchunguzi huo wa maoni uliofanyika kati ya Machi 15 hadi 17 ni asilimia 41 tu ya waliotoa maoni yao walisema, watamapigia kura Trump.
Uchaguzi wa rais wa Marekani utafanyika tarehe 3 Novemba mwaka huu.../