May 07, 2020 17:09 UTC
  • Ripoti ya kushtusha: Wengi waliofariki dunia kwa Corona nchini Uingereza, ni Waingereza Weusi

Matokeo ya uchunguzi mpya uliofanywa nchini Uingereza yanaonyesha kwamba Waingereza weusi ndio wanaongoza kwa kufariki dunia kutokana na virusi vya Corona kati ya watu wa jamii nyingine.

Hayo yamethibitishwa leo na David Lammy, Waziri Kivuli wa Sheria wa chama cha Leba nchini Uingereza ambapo ameitaja ripoti ya uchunguzi uliofanywa na ofisi ya takwimu ya taifa nchini humo kwamba ni ya kushangaza na kushtusha na ameitaka, serikali ya London kuchukua hatua za lazima za kuwalinda wanawake na wanaume wenye asili ya Afrika pamoja na watu wa jamii za walio wachache kutokana na virusi hatari vya Corona. Matokeo ya kushtusha yanayotokana na uchunguzi wa ofisi ya takwimu ya taifa yanaonyesha kwamba hatari ya kufariki dunia wanaume na wanawake weusi ni mara nne zaidi ya wagonjwa wengine wa Corona. Kadhalika ripoti hiyo imeeleza kwamba raia wa Bangladesh, Pakistan na India nao pia wako katika hatazi zaidi ya kupoteza maisha kutokana na virusi vya Corona, kuliko watu wengine.

David Lammy, Waziri Kivuli wa Sheria wa chama cha Leba nchini Uingereza

Takwimu ya vifo vinavyotokana na virusi hivyo hatari vya Corona katika maeneo ya watu masikini na ya watu wa jamii za wachache nchini Uingereza, ni mara mbili zaidi ya maeneo ya mengine. Kwa sasa serikali ya Uingereza inakabiliwa na mashinikizo makali ya fikra za walio wengi ikitakiwa kufanya uchunguzi kuhusiana na ubaguzi uliopo katika sekta ya afya wakati huu wa ugonjwa wa Covid-19. Ripoti za kushtua pia zinaonyesha kufariki dunia kwa asilimia 72 ya madaktari wa jamii za walio wachache nchini Uingereza, suala ambalo limezidisha hali ya suitafahamu. Kuhusina na suala hilo Wizara ya Afya ya Uingereza imeikabidhi kamati maalumu kuanzisha uchunguzi. Pamoja na hayo chama cha Leba kimetaka kuundwa kamisheni huru kuchunguza matokeo ya kijamii na kiuchumi yanayosababishwa na ubaguzi wa sekta ya afya na pia kufikia kupungua matumaini ya kuishi kwa watu baadhi.

Tags