Watu 47 wafariki dunia katika mapigano mapya nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61087-watu_47_wafariki_dunia_katika_mapigano_mapya_nchini_afghanistan
Watu 47 wamefariki dunia katika mapigano mapya kati ya jeshi la serikali ya Afghanistan na wanachama wa kundi la Taleban katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 20, 2020 00:50 UTC
  • Watu 47 wafariki dunia katika mapigano mapya nchini Afghanistan

Watu 47 wamefariki dunia katika mapigano mapya kati ya jeshi la serikali ya Afghanistan na wanachama wa kundi la Taleban katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imetangaza kwamba, wanachama 11 wa kundi la Taleban waliuawa katika mapigano yaliyojiri katika viunga vya mji wa Kunduz, kaskazini mwa nchi hiyo, huku watu wanane wengine wakijeruhiwa. Kadhalika jeshi la serikali ya Afghanistan limefanikiwa kusambaratisha shambulizi la wanachama wa Taleban katika mji huo wa Kunduz. Aidha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imetangaza habari ya kuuawa wanachama 15 wa kundi hilo katika mapigano na maafisa wa jeshi la serikali katika jimbo la Logar, Zabul na Herat.

Taleban

Katika upande mwingine wanachama wa Taleban waliopenyeza kati ya polisi katika moja ya vituo vya jimbo la Kunduz, wametekeleza shambulizi ambalo limeua polisi watano na wengine saba kujeruhiwa. Khalil Asir, Msemaji wa Jeshi la Polisi katika jimbo la Takhar amesema kuwa, watu sita miongoni mwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali ya nchi hiyo wameuawa katika shambulizi lililotekelezwa na wanachama wa Taleban katika mji wa Baharak, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Aidha Hanif Rezai, msemaji wa kamandi ya jeshi kaskazini mwa Afghanistan amenukuliwa akisema kuwa, jumla ya wanachama tisa wa kundi la Taleban wameuawa katika shambulizi la anga lililotekelezwa na jeshi katika ngome ya wanachama wa kundi hilo katika mji wa Qush Tappeh wa jimbo la Jowzjan.