Mwandamanaji auawa Marekani katika maandamano ya kulalamikia muaji
Mtu mmoja amepigwa raisasi na kuuawa katika maandamano katika mji wa Minneapolis nchini Marekani.
Mtu huyo ameuawa katika maandamano ya kulalamikia kifo cha Mmarekani mwenye asili ya Afrika ambaye alipoteza maisha mikononi mwa polisi mjini humo.
Maandamano hayo yaliendelea Jumatano usiku kwa siku ya pili mfululizo huku wananchi wenye hasira wakilaumu polisi kwa kuwakandamiza Wamarekani wenye asili ya Afrika. George Floyd, aliyekuwa na umri wa miaka 46 alipoteza maisha Mei 25 wakati polisi alipopiga goti kwenye shingo lake kwa dakika nane hadi alipopoteza maisha.
Meya wa Minneapolis Jacob Frey amesema afisa huyo wa polisi na wenzake wawili walifutwa kazi Jumanne na kwamba watafunguliwa mashtaka ya jinai.
Maandamano ya kupinga ukatili huo wa polisi pia yameripotiwa katika jimbo la California.
Video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Marekani, imemuonyesha polisi huyo mzungu akiwa amemlaza chini kifudifudi mtu huyo huku akiwa amemkandamiza vibaya shingo lake kwa goti lake la mguu wa kushoto.
Mtu huyo mwenye asili ya Afrika aliyejulikana kwa jina la George Floyd alikuwa akipiga kelele kwa kusema: "Umenibana shingo siwezi kupumua" "Naomba maji" na "Usiniue" hadi alipofariki dunia.
Mauaji ya kiholela ya Wamarekani wenye asili ya Afrika ambayo yanatekelezwa na polisi wazungu nchini Marekani yameongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni nchini humo.
Siku ya Jumatano Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ililaani vikali ukatili huo wa polisi ya Marekani uliopelekea kupoteza maisha raia mwengine mwenye asili ya Afrika.