Waislamu wa Marekani wapaza sauti kulaani ubaguzi, ukatili wa polisi
Mashirika ya Waislamu nchini Marekani yamejiunga na wimbi la malalamiko ya kuishinikiza serikali ya Washington ifanye mageuzi haraka iwezekanavyo kwa ajili ya kuondoa ubaguzi wa rangi wa kimfumo katika muundo wa polisi ya nchi hiyo.
Katika taarifa ya pamoja kwa niaba ya Waislamu wa Marekani, mashirika 95 ya kiraia kutoka majimbo 30 ya Marekani yakiongozwa na Chama cha Mawakili Waislamu nchini humo yamesema, "vitendo vya kunyanyaswa na kukandamizwa Waislamu weusi ambao hawana silaha vina historia ndefu ya kutisha."
Mashirika hayo yameeleza bayana kuwa, "sisi kama Waislamu wa Marekani, pasina kujali tofauti zetu za kijamii, tutatumia nguvu zetu na ukakamavu wetu kushinikiza mageuzi haya katika idara ya polisi, kwa kuwa maisha ya watu weusi ni muhimu pia."
Asasi hizo za kiraia za Waislamu wa Marekani zimesema haziwezi kunyamazia kimya jinai hizo za kuchupa mipaka za polisi ya Marekani dhidi ya watu weusi, kwani Waislamu nchini humo wamekuwa wahanga wakuu wa unyanyasaji huo kwa miaka mingi sasa.
Kwa karibu wiki tatu sasa, miji na majimbo mbalimbali ya Marekani yanashuhudia maandamano na ghasia kubwa za kulalamikia vitendo vya ubaguzi wa rangi vya polisi wa nchi hiyo kufuatia kuuliwa kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika kwa jina la George Floyd.
Maandamano haya ya kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi yanashuhudiwa pia katika nchi mbalimbali duniani, hususan za Ulaya.