Jul 11, 2020 11:33 UTC
  • Ubelgiji yaendelea kushuhudia maandamano ya kulaani marufuku ya hijabu

Kwa siku kadhaa sasa, mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels umeshuhudia maandamano ya kulaani marufuku ya uvaaji hijabu na mitandio ya kichwani katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za nchi hiyo ya Ulaya.

Maelfu ya waandamanaji hao wamekuwa wakibeba mabango yenye jumbe zisemazo: Ondoa mikono yako kwenye mitandio yangu, Haki Yangu na Basi Tena.

Waandamanaji hao wamekosoa vikali uamuzi uliotolewa na mahakama moja nchini humo mnamo Juni 4, ukipiga marufuku uvaaji wa 'nembo za kidini' ikiwemo hijabu katika taasisi za elimu ya juu za nchi hiyo.

Baraza la Waislamu Ulaya (CEM) limekosoa vikali uamuzi huo na kubainisha kuwa, "ni masikitiko baadhi wanalazimishwa kuvua hijabu ili wapate elimu."

Mwanachuo aliyevaa hijabu nchini Ubelgiji

Disemba mwaka jana, Mahakama ya Rufaa ya Ubelgiji iliidhinisha uamuzi wa kupiga marufuku uvaaji mitandio ya kichwa skulini katika moja ya maeneo ya nchi hiyo. Tangu mwaka 2013, taasisi moja ya serikali ya Ubelgiji ilipiga marufuku uvaaji mitandio mashuleni.

Hata hivyo mwaka 2018, wazazi wa wanafunzi 11 katika eneo la Limburg walifungua kesi ya malalamiko kupinga marufuku hiyo ya uvaaji mitandao ya kichwa na wakafanikiwa kushinda kesi hiyo.

Serikali na mahakama za nchi mbali mbali za Ulaya zimekuwa zikipitisha sheria kali dhidi ya raia Waislamu wa nchi hizo.

Tags