Uingereza yaionya tena Washington kuhusu kesi ya jasusi wa Marekani
Kwa mara nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ameionya Washington kuhusu kesi ya jasusi wa nchi hiyo ambaye amemuua kijana mmoja raia wa Uingereza na kukimbilia Marekani.
Serikali ya London imeitaka White House imkabidhi mtuhumiwa huyo kwa Uingereza ingawa haikusema itachukua hatua gani iwapo haitokabidhiwa jasusi huyo. Onyo hilo limetolewa wakati huu wa kukabiria mazungumzo baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Uingereza.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab amesema, uadilifu haukutendeka kuhusu suala hilo hivyo London inaitaka Marekani imkabidhi mtuhumiwa huyo anayejulikana kwa jina la Anne Sacoolas kwa Uingereza ili uadilifu uweze kutendeka.
Bi Anne Sacoolas, (42) ameondoka nchini Uingereza na kukimbilia Marekani licha ya awali kudai kwamba hakuwa na nia ya kuondoka nchini humo. Taarifa zinasema kuwa, siku ya tukio Bi Sacoolas aliondoka na gari katika kituo cha kijeshi cha Marekani cha RAF Croughton mjini London na kuendesha gari upande sio kabla ya kumgonga kijana mmoja wa miaka 19 raia wa Uingereza na kumuua.
Gazeti la The Sun la Uingereza nalo limeripoti habari hiyo na kufichua kwamba, Bi Anne Sacoolas ni jasusi wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na amefanikiwa kutoka Uingereza na kukimbilia Marekani akidai kuwa na hadhi ya kidiplomasia.
Kwa upande wake shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, mume wa Anne Sacoolas naye ni jasusi wa Marekani anayefanya kazi katika kituo cha anga cha Marekani kiitwacho RAF Croughton mjini London.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema London inaitaka Marekani imrejeshe Uingereza jasusi huyo hasa kwa vile mahakama ya Uingereza imempata na hatia ya kuendesha gari kwa namna ya hatari, tena upande usio sahihi na kumuua kijana wa Uingereza anayejulikana kwa jina la Harry Dunn.
Baadhi ya vyombo vya habari vimetangaza kuwa, Marekani ni nchi isiyo na mwamana hata kidogo na haisiti kumletea madhara hata muitifaki wake wa karibu sana.