Kuendelea ushirikiano wa Iran na Venezuela licha ya vitisho vya Marekani
(last modified Thu, 06 Aug 2020 06:27:55 GMT )
Aug 06, 2020 06:27 UTC
  • Kuendelea ushirikiano wa Iran na Venezuela licha ya vitisho vya Marekani

Ushirikiano wa kibiashara na kisiasa wa Iran na Venezuela unaendelea kuimarika licha ya kuwepo vitisho na vikwazo vya Marekani. Kutumwa meli za mafuta za Iran nchini Venezuela mwezi uliopita ilikuwa hatua ya kwanza katika uwanja huo na sasa Iran imechukua hatua nyingine ya kufungua duka kubwa la bidhaa zake katika mki mkuu wa nchi hiyo, Caracas.

Akizungumzia ufunguzi wa duka hilo, Ruben Dario Molina, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema hiyo ni hatua nyingine muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi mbili katika kukabiliana na siasa za mabavu za Marekani. Molina amesema ufunguzi wa duka hilo lililopewa jina la Megasis umetimia katika hali ambayo Marekani imezidisha mashinikizo na vikwazo dhidi ya Venezuela tena katika mazingira haya magumu ya kuenea virusi vya corona. Amesema ufunguzi wa duka hilo kubwa la bidhaa za Iran ni hatua yenye umuhimu mkubwa kwa sababu biashara zinapasa kufanyika ili kumuhudumia mwanadamu na kwa maslahi ya nchi mbili.

Duka hilo la bidhaa za Iran limefunguliwa kutokana na uwekezaji wa pamoja wa nchi mbili wa dola milioni 10 ambapo karibu mashirika 150 ya Venezuela yameshirikishwa katika mradi huo muhimu wa kibiashara. Bidhaa zaidi ya 250 za Iran zinauzwa katika dula hilo kubwa.

Duka la bidhaa la Megasis limefunguliwa katika hali ambayo nchi mbili za Iran na Venezuela ziko chini ya mashinikizo na vikwazo vikali vya Marekani. Ni miaka kadhaa sasa ambapo viongozi wa Marekani wameiwekea Venezuela vikwazo vikali vya kiuchumi na kisiasa kwa lengo la kuzidisha matatizo ya nchi hiyo na hatimaye kuiangusha serikali halali ya Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo.

Maafisa wa Iran na Venezuela wakishiriki ufunguzi wa duka la Magasisi mjini Caracas

Kwa hakika viongozi wa Marekani hawawezi kuvumilia kuona siasa za uadilifu na za kupambana na ukoloni zikitekelezwa na serikali ya mrengo wa kulia nchini Venezuela kwa sababu hilo lina maana ya kukatwa mikono ya uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Carlos Ron Martinez, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela anayeshughulikia masuala ya Amerika ya Kaskazini amesema lengo la vikwazo vya kadhalimu vya Marekani dhidi ya Venezuela katika mazingira haya ya kuenea virusi vya corona ni kuwashinikiza viongozi wa nchi hiyo na hatimaye kuwandoa madarakani.

Licha ya kutekelezwa siasa za vikwazo na vitisho za Marekani dhidi ya Venezuela lakini siasa hizo hazijafanikiwa kufikia malengo maovu yanayokusudiwa na watawala wa Washington na badala yake  Rais Nicolas Maduro amefanikiwa pakubwa katika kusimama imara mbele ya siasa hizo za mabavu na kuweza kudhibiti vizuri mgogoro wa kisiasa na kiuchumi unaochochewa na maadui dhidi ya nchi yake.

Katika upande wa pili, Michael Kozak, naibu mkuu wa Ofisi ya Amerika ya Latini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema kwamba kila aina ya uwepo wa Iran katika eneo la Amerika ya Latini haiwafurahishi viongozi wa Marekani. Amesema bila shaka kufunguliwa kwa duka kubwa la bidhaa za Kiirani huko Caracas ni dhihirisho la umoja na ushirikiano wa nchi mbili.

Watawala wa Marewkani wanatekeleza na kusisitiza kuendeleza vikwazo dhidi ya nchi nyingine za dunia katika mazingira haya ya kuenea virusi vya corona katika kila pembe ya dunia, ikiwemo Venezuela, na hii ni katika hali ambayo viongozi wa mashirika muhimu ya kimataifa ikiwemo Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, wametaka kuondolewa vikwazo hivyo vya kiuchumi ili kuzipa nchi tofauti uwezo wa kuweza kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo hatari kwa maisha ya mwanadamu.

Raia wa Venezuela wakinunua bidhaa katika duka la Megasis

Ni kwa msingi huo ndipo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikapuuzilia mbali vikwazo hivyo vya Marekani na kuamua kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na Venezuela kupitia hatua ya hivi karibuni ya kufungua duka kubwa la bidhaa zake, vikiwemo vyakula, nguo na madawa huko Caracas ili kupunguza matatizo yanayowakabili wananchi wa nchi hiyo kutokana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani.

Katika uwanja huo, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameishukuru sana serikali na taifa la Iran kutokana na mchango wake kwa watu wa nchi hiyo na kusisitiza kwamba Venezuela haijaachwa peke yake bali ina marafiki shujaa ambao wamesimama pembeni yake.

Hata kama watawala wa Marekani wangali wanapiga ngoma ya vikwazo na vitisho dhidi ya nchi nyingine zinazojitawala, ni wazi kuwa kuwepo ushirikiano wa aina hiyo baina ya mataifa tofauti ni ishara inayothibitisha kwamba nchi shujaa kama vile Iran kamwe hazitatishwa na ubeberu wa Marekani.

Tags