Marekani na wizi wa mafuta ya Syria
(last modified Fri, 28 Aug 2020 02:22:00 GMT )
Aug 28, 2020 02:22 UTC
  • Marekani na wizi wa mafuta ya Syria

Nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki zimetoa taarifa ya pamoja mwishoni mwa kikao cha tatu cha Kamati ya Katiba ya Syria zikilaani wizi wa mafuta unaofanywa na Marekani nchini Syria.

Mafuta ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya pato la kigeni la serikali ya Syria. Kabla ya kuanza vita na makundi ya kigaidi hapo mwaka 2011, Syria ilikuwa ikizalisha karibu mapipa laki 3 na 80 elfu kwa siku. Kwa sasa Marekani na makundi ya wanamgambo wa Kikurdi wanaofadhiliwa na nchi hiyo wanadhibiti maeneo yenye utajiri wa mafuta ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Syria. Hivi karibuni kampuni moja ya Marekani ilisaini mkataba na kundi la waasi wa Kikurdi la Syrian Democratic Forces (SDF) kuhusiana na maneo yenye utajiri wa mafuta yanayodhibitiwa na kundi hilo, na mkataba huo umeungwa mkono na kupasishwa na serikali ya Marekani.

Seneta Lindsey Graham wa chama cha Republican hivi karibuni pia alitangaza kuwa, kamanda wa kundi la Syrian Democratic Forces, Mazloum Abdi amemjulisha kwamba kundi hilo limesaini makubaliano ya kuchimba mafuta huko mashariki mwa Syria na kampuni moja ya Kimarekani, na kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, ameuunga mkono na kupasisha mkataba huo.

Marekani na wanamgambo wa Kikurdi wametangaza kuwa wamesaini mtakaba huo kwa shabaha ya "kusasisha" visima hivyo vya mafuta. Hata hivyo inaonekana kuwa, lengo muhimu la Marekani la kupora na kutwaa mafuta ya Syria kinyume cha sheria ni kuzidisha uwezo wa kifedha wa makundi hayo ya waasi wa Kikurdi nchini Syria. Maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi huko kaskazini mashariki mwa Syria yanazalisha mapipa elfu 45 ya mafuta kwa siku ambayo yana thamani ya dola milioni 800 kwa bei ya dola 50 kwa kila pipa moja la mafuta. Fedha hizo zinaweza kuwa pato zuri kwa makundi ya waasi wa Kikurdi. 

Wamarekani wanapora mafuta ya Syria

Nukta muhimu zaidi ni kwamba, kwa kuuza mafuta ya maeneo ya kaskazini mashariki mwa Syria na kuzidisha uwezo wa kifedha wa makundi ya waasi, Washington inataka kuzidisha mielekeo ya kutaka kujitenga makundi hayo ya wanamgambo waasi. Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Marekani, Jonathan Rath Hoffman alisema mwezi Oktoba mwaka jana kwamba: Pato la mafuta hayo halichukuliwi na Marekani, bali wanapewa wapiganaji wa kundi la Syrian Democratic Forces. Kwa msingi huo uwezo huu wa kifedha unatayarisha mazingira mazuri ya kutekeleza mpango wa kuigawa Syria au kwa uchache kuanzishwa utawala wa mfumo wa federali nchini Syria ambapo Wakurdi wataunda sehemu moja ya federesheni hiyo. Suala la kudhoofisha serikali kuu ya Syria ni miongoni mwa malengo ya kistratijia ya Marekani, na hapana shaka kuwa, kuyawezesha kifedha makundi ya waasi nchini humo kunafanyika kwa shabaha ya kuyaimarisha zaidi mkabala wa serikali ya Damascus.

Nukta nyingine ya kuashiria hapa ni kuwa Marekani yenyewe inatwaa na kupora sehemu nyingine ya mafuta ya maeneo ya mashariki mwa Syria. Hivi karibuni Wizara ya Ulinzi ya Russia iliashiria wizi wa mafuta ya Syria unaofanywa na Marekani na kutangaza kuwa: Biashara inayofanywa na Marekani ya mafuta ya Syria inaipatia nchi hiyo faida ya dola milioni 30 kwa mwezi.

Inaonekana kuwa, Wamarekani ambao wanaliangalia eneo la magharibi mwa Asia kwa jicho la faida za kimaada, hasa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuitaja Saudi Arabia kuwa ni "gombe la kukamua maziwa", wanadhamini gharama za kuwepo wanajeshi wao katika eneo hilo kwa kuiba na kupora utajiri wa mafuta ya Syria.

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana Donald Trump alisema kuwa, licha ya wanajeshi wa Marekani kuondoka kaskazini mashariki mwa Syria lakini idadi ndogo ya wanajeshi hao itabakia katika maeneo yenye utajiri wa mafuta ya Syria. Trump alidai kuwa wanajeshi hao watabakia Syria kwa shabaha ya kulinda visima vya mafuta vya nchi hiyo.

Sasa imebainika kuwa, madai ya kulinda visima vya mafuta nchini Syria ni wenzo tu unaotumiwa kwa ajili ya kudhamini fedha za kugharamia uwezpo wa vikosi vya majeshi ya Marekani katika eneo la magharibi mwa Asia na kuimarisha misimamo ya kutaka kujitenga nchini Syria.

Marais Hassan Rouhani wa Iran (kushoto) Erdogan wa Uturuki na Vladmir Putin wa Russia

Kwa kutilia maanani malengo hayo habithi, nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki zimetoa taarifa zikilaani hatua ya Marekani ya kupora mafuta ya Syria na kutangaza kuwa mafuta hayo ni mali ya taifa na watu wa nchi hiyo.