Wabunge Amerika ya Latini wataka kususiwa utawala wa Kizayuni
Wabunge wa baadhi ya nchi za Amerika ya Latini wametaka kutungwe sheria za kuususia na kuuwekea vikwazo utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na mpango wa utawala huo ghasibu wa kutaka kuteka ardhi zaidi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Mtandao wa habari wa "al Arabi 21" umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wabunge wa nchi sita za Amerika ya Latini wamesema hayo katika kongamano la "Jumuiya ya Mabunge kwa ajili ya Quds" na kutilia mkazo wajibu wa kutungwa sheria za kuususia utawala wa Kizayuni.
Wabunge hao wamesema, mabunge yana nafasi muhimu katika utungaji sheria ya kuisusia na kuiwekea vikwazo Israel kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina.
Wamesema, mapambano ya kulihami taifa la Palestina yanahitajia kuchukuliwa hatua za kivitendo ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku kuingia bidhaa za Israel katika nchi za Amerika ya Latini.
Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni amekuwa akisisitiza kutekeleza njama zake za kuteka ardhi zaidi za Wapalesitna za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan licha ya baadhi ya nchi za Kiarabu kama Umoja wa Falme za Kiarabu kujikomba kwa Wazayuni kupitia kutangaza rasmi uhusiano wao wa kidiplomasia na utawala huo dhalimu.
Dunia nzima inapinga njama za Wazayuni za kutaka kuteka ardhi zaidi za Wapalestina. Hata Umoja wa Mataifa nao unapinga njama hizo, upinzani ambao hatimaye umezaa matunda na kumuogopesha Benjamin Netanyahu ambaye mwishowe amelazimika kuakhirisha utekelezaji wa njama hizo.