AI yataka kufanyike uchunguzi huru kuhusu mauaji ya kikatili ya Khashoggi
Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International jana Ijumaa lilitoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru wa kimataifa na usiopendelea upande wowote kuhusu mauaji ya kikatili aliyofanyiwa mwandishi Jamal Khashoggi katika ubalozi wa Saudi Arabia nchini Uturuki.
Kwa mujibu wa gazeti la "al Arabi 21," shirika la Amnesty International limesema katika taarifa yake kwamba kuna wajibu wa kupandishwa kizimbani na kuhukumiwa watuhumiwa wote wa mauaji ya Khashoggi kwani usikilizaji wa kesi za baadhi ya watu hao ulifichwafichwa na haukufanyika kwa uwazi. Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa, hukumu ya mwisho iliyotolewa ya kesi hizo ilipuuza kuhusika viongozi wa Saudia katika jinai hiyo ya kutisha na hata haikusema mwili wa marehemu umepelekwa wapi.
Naye Agnes Callamard, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mauaji yanayofanyika nje ya mipaka ya sheria alisema siku ya Jumatatu kwamba mchakato wa kusikilizwa kesi za wauaji wa Khashoggi na hukumu zilizotolewa ni sawa na kuuchezea shere uadilifu. Alisema mchakato wa kusikiliza kesi hiyo ulikosa insafu, uadilifu na uwazi.
Jumatatu iliyopita, mwendesha mashtaka mmoja wa Saudi Arabia alitoa taarifa na kudai kuwa faili la upande mahsusi wa uhalifu wa mauaji ya Jamal Khashoggi limefungwa kutokana na watu wa familia ya Khashoggi kuamua kusamehe na upande wa faili la umma la wahalifu hao ni kwamba watu watano amefungwa miaka 20 kila mmoja, wawili miaka 10 na mmoja miaka saba jela.
Khashoggi ni miongoni mwa watu waliokuwa wanasakwa na viongozi wa Saudi Arabia ili auawe kutokana na ukosoaji wake na hatimaye aliuliwa kikatili katika ubalozi wa Saudia nchini Uturuki.