Biden: Nitakomesha fujo zote za Trump
Mgombea wa kiti cha urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic amekosoa hali ya mambo ya nchi hiyo hivi sasa wakati wa uongozi wa hasimu wake wa chama cha Republican Donald Trump.
Joe Biden mgombea wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Marekani ametuma jumbe kadhaa katika ukurasa wake wa twitter akikosoa hali ya mambo ya nchi yake chini ya uongozi wa Rais Donald Trump. Katika ujumbe wake wa kwanza Biden amekosoa hali ya mambo ya sasa nchini Marekani na kusema na hapa ninamnukuu: "Naahidi kuwa nitahitimisha ghasia za Trump na kupatia ufumbuzi hali hiyo ya mambo."
Aidha katika ujumbe wake wa pili mgombea huyo wa kiti cha urais wa chama cha Democratic amesema: Zaidi ya wananchi wa Marekani karibu laki mbili na nusu wameaga dunia kwa maradhi ya Covid-19 na Rais Trump ameshindwa kuchukua hatua kudhibiti maafa hayo.
Joe Biden amesisitiza pia juu ya umuhimu wa Afya na Tiba kwa kusema: Mimi nitakulindeni kama ninavyoilinda familia yangu.
Joe Biden ametuma jumbe hizo huku mchuano kuelekea uchaguzi wa rais nchini Marekani ukizidi kupamba moto kati yake na Trump.