Nov 07, 2020 07:33 UTC
  • Indhari ya WFP na FAO kuhusu baa la njaa katika nchi kadhaa duniani

Mashirika ya Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) yametahadharisha kuhusu njaa katika maeneo kadhaa duniani.

Ripoti ya FAO imesema mamilioni ya watu katika nchi nne zilizoghubikwa na tatizo la kutokuwa na uhakika wa chakula za Burkina Faso, Kaskazini mwa Nigeria, Sudan Kusini na Yemen wanahitaji msaada wa chakula ili kuepuka kutumbukia katika baa kubwa la njaa.

Akizungumza Ijumaa mjini Geneva Uswisi kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao Claudia Ah Poe, mshauri wa ngazi ya juu wa WFP amesema, “Tunatiwa hofu kwamba watu hawa wanaweza kukabiliwa na hatari kubwa ya baa la njaa endapo hali itaendelea kuzorota katika miezi ijayo.” 

Kupitia taarifa ya pamoja na  FAO, shirika la WFP pia limeonya kwamba nchi zingine 16 zinakabiliwa na dharura kubwa ya chakula au msururu wa dharura katika mieszi mitatu hadi sita ijayo.

Mtoto Myemeni akiwa katika hali mbaya kutokana na ukosefu wa chakula uliosababishwa na hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen

Mashirika hayo katika ripoti yao mpya kuhusu kutokuwa na uhakika wa chakula katika maeneo hayo manne yamesema chachu kubwa ya migogoro hii ya kibinadamu ni pamoja na vita vinavyoendelea na ukosefu wa fursa za kibinadamu zinazohitajika katika jamii, mabadiliko ya  tabianchi na mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na janga la corona au COVID-19.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, sera za kivita za nchi za Magharibi, hasa Marekani na waitifaki wao, zimeibua vita, magaidi na migogoro katika nchi nyingi duniani na hivyo kusababisha matatizo mengi hasa ukosefu wa chakula.

 

Tags