Russia: Mshindi wa uchaguzi wa Marekani hajatangazwa rasmi hivyo hatutumi pongezi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i64600-russia_mshindi_wa_uchaguzi_wa_marekani_hajatangazwa_rasmi_hivyo_hatutumi_pongezi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa nchi yake kwa sasa haimpongezi mgombea yeyote wa uchaguzi wa rais wa Maekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2020 07:48 UTC
  • Russia: Mshindi wa uchaguzi wa Marekani hajatangazwa rasmi hivyo hatutumi pongezi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa nchi yake kwa sasa haimpongezi mgombea yeyote wa uchaguzi wa rais wa Maekani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Interfax, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amekumbusha kuwa, bado matokeo rasmi ya uchaguzi wa rais wa Marekani hayajatangazwa na kuongeza kuwa: "Kwa kuzingatia kuwa mshindi bado hajajulikana, Russia haijatuma salamu za pongezi kwa yeyote."

Siku kadhaa zilizopita Lavrov alisema kuna mfarakano mkubwa katika mfumo wa utawala wa Marekani na kusema: "Hadi sasa ni vyombo vya habari tu ndivyo vimetangaza matokeo ya upigaji kura wa Marekani na hakuna taarifa sahihi na rasmi kuhusiana na uchaguzi huo."

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Lavrov ameongeza kuwa, iwapo Biden atatangazwa mshindi atafuata sera za rais wa zamani wa Marekani Barack Obama.

Russia imekuwa ikituhumiwa kuwa iliingilia uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016 na kuathiri matokeo ya uchaguzi huo. Wakuu wa Russia wamepinga vikali tuhuma hizo.

Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump na mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican amepinga matokeo ya uchaguzi ambayo hadi sasa yanaonyesha kuwa Joe Biden ameshinda. Trump amedai mara kadhaa kuwa kumekuwepo na wizi mkubwa wa kura katika uchaguzi huo wa rais.