Wasiwasi wa kuongezeka njaa na umasikini nchini Marekani
(last modified Wed, 23 Dec 2020 00:52:57 GMT )
Dec 23, 2020 00:52 UTC
  • Wasiwasi wa kuongezeka njaa na umasikini nchini Marekani

Kusambaa virusi vya Corona nchini Marekani na mazingira yaliyosababishwa na utendaji mbovu wa serikali ya nchi hiyo ni mambo ambayo yamepelekea kuongezeka matatizo ya kijami na kiuchumi yanayoikabili nchi hiyo.

Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba, Kamala Harris Makamu wa rais mteule wa Marekani ametahadharisha kuhusiana na kuongezeka baa la njaa nchini humo. Bi Harris sanjari na kuashiria kwamba, katika kila familia saba katika jimbo la Georgia basi familia moja inataabika kwa njaa amesisitiza kuwa: Tunashuhudia mgogoro wa njaa nchini Marekani na kuna familia nyingi zinazoteseka na kutaabika kwa njaa huku katika kila familia sita, familia moja ikiwa inakabiliwa na tatizo la kushindwa kodi ya nyumba.

Baa la njaa na kuongezeka umasikini limegeuka na kuwa tatizo kubwa linaloikumba Marekani kwa sasa. Utendaji mbovu wa serikali ya Rais Donald Trump ambaye siku zake za kubakia Ikulu ya White House zinaelekea ukingoni katika kudhibiti maradhi ya Covid-19, kukana kwake kuweko virusi hivyo katika nyakati tofauti na wakati huo huo kutoafiki kutekelezwa karantini ya muda mrefu, uhaba wa zana na vifaa vya tiba vinavyohitajika sambamba na gharama kubwa za matibabu ni mambo ambayo yameifanya Marekani iwe nchi iliyoathiriwa zaidi na virusi vya Corona baada ya raia karibu milioni 18.5 kuambukizwa na wengine karibu lakini 3 na nusu kuaga duniani kwa maradhi hayo.

Ombaomba nchini Marekani wameongezeka

 

Hali hii imeifanya Marekani ikumbwe na mgogoro mkubwa wa kiuchumi, maelfu ya Wamarekani kukosa ajira na kuongezeka umasikini na tofauti za kimatabaka katika nchi hiyo.

Daniel Kwak, mwanasheria na wakili mtetezi wa masuala ya haki za binadamu anasema kuhusiana na suala hilo: Kabla ya kuibuka virusi vya corona, pengo la masikini na tajiri nchini Marekani ndilo lililokuwa kubwa zaidi katika ulimwengu wa Magharibi. Hivi sasa tofauti hiyo imeongezeka zaidi. Tabaka la matajiri limeyatumia maradhi haya kwa ajili ya kujilimbikkizia zaidi utajiri na hivyo kuwafanya mamilioni ya wananchi wa nchi hiyo kuwa masikini.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, tangu vilipoingia virusi vya corona nchini Marekani, njaa na umasikini katika miji mbalimbali ya nchi hiyo viliongezeka maradufu. Mathalani, katika jiji la New York idadi ya watu waliokuwa wakitaabikka kwa njaa na kutokuwa na usalama wa chakula iliongezeka mara mbili na kufikia takribani milioni mbili. Kadhalika kufungwa na kusimamishwa baadhi ya shughuli nchini Marekani kutokana na kusambaa virusi vya corona kulipelekea kuongezeka idadi ya watu wanaohitajia vifurushi vya misaada ya chakula.

Rais Donald Trump wa Marekani

 

Gazeti la New York Times limeripoti kuwa, watoto milioni 18 ambao ni sawa na moja ya nne (robo) ya watoto wote wa nchi hiyo yamkini wakahitajia msaada wa chakula ambapo kiwango hiki kimeongezeka kwa asilimia 63 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Adam Schiff, Mwenyekiti wa Kamati ya Upelelezi ya Bunge la Marekani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Kuongezeka kiwango cha njaa nchini Marekani ni ishara ya wazi ya kushindwa  na kufeli vibaya nchi hiyo katika uandaaji wa sera zake.

Huku hali ikiwa ni hiyo, katika mwaka huu wa 2020 pekee, dola bilioni 740 zilitengwa kama bajeji ya kijeshi ya nchi hiyo. Katika miaka 20 ya hivi karibuni zaidi ya dola trilioni 10 za walipa kodi nchini Marekani zimetumika katika masuala ya kijeshi na vita. Katika vita vya Marekani vya baada ya Septemba 11, 2001 pekee, nchi hiyo imetumia moja kwa moja takribani dola trilioni 8 ambapo ikijumuishwa na gharama nyingine zisizokuwa za moja kwa moja za vita hivyo, inaonekana kuwa, karibu dola trilioni 40 za rasilimali ya Wamarekani zimetumika kwa ajili ya chokochoko za kijeshi nje ya mipaka ya nchi hiyo.

Joe Biden, rais mteule wa Marekani

 

Hii ni katika hali ambayo, kama ingetengwa japo asilimia 10 tu ya fedha hizo na kutumika kwa ajili ya kushughulikia tatizo la njaa na umasikini nchini Marekani au zingetumika kwa ajili ya kukarabati miundomsingi iliyochakaa ya nchi hiyo, basi hii leo taifa hilo lisingekuwa linataabika na kuandamwa na matatizo haya linayokabiliwa nayo hivi sasa.

Pamoja na hayo, wapenda vita ambao wanafahamika kama 'wenye hisa ya vita' kwao wao umwagaji damu na mauaji katika nukta ya mbali kabisa ya dunia ni muhimu zaidi kuliko kuondoa umasikini unaowakabili mamilioni ya wananchi wa Marekani. Katika hili hakuna tofauti ya hivyo baina ya wanasiasa wa chama cha Republican na wale wa Democrat.