Jan 04, 2021 03:29 UTC
  • Kupinga Marekani kupasishwa bajeti ya Umoja wa Mataifa

Katika kipindi cha uongozi wake, Rais Donald Trump wa Marekani ameukosoa mara chungu nzima Umoja wa Mataifa pamoja na utendaji wake na hata kutishia kupunguza msaada wa nchi yake kwa asasi hiyo ya kimataifa.

Hivi sasa Marekani ikitumia visingizio visivyo na maana imekwamisha kupasishwa bajeti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa.

Kelly Craft, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Alkhamisi iliyopita aliupigia kura ya hapana mchakato wa kuidhinisha bajeti ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mwaka huu wa 2021. Craft alidai katika kikao cha Umoja wa Mataifa cha kuidhinisha bajeti ya umoja huo kwamba, bajeti hiyo ya Umoja wa Mataifa iko dhidi ya Israel na kwamba, hakujachukuliwa hatua za kutosha kwa ajili ya uangalizi na usimamizi wa silaha za Iran. Aidha alisema kuwa, Marekani itachukua hatua kwa mujibu wa mitazamo yake.

Bajeti ya Umoja wa Mataifa katika miaka ya nyuma imekuwa ikipasishwa kwa kauli moja na nchi wanachama wa umoja huo.  Katika kikao cha Jumatano iliyopita cha Kamati ya Bajeti ya Umoja wa Mataifa, Marekani ilipiga kura ya hapana pia kwa mpango wa bajeti ya umoja huo.

Donald Trump

 

Inaonekana kuwa, hatua ya hivi karibuni ya Marekani ya kupinga bajeti ya Umoja wa Matifa ya mwaka huu wa 2021 inalenga kuishinikiza taasisi hiyo ya kimataifa  iungane nayo katika matakwa yake yasiyokuwa ya kishieria.

Kwa upande mmoja, serikali ya Trump ambayo inavuta pumzi zake za mwisho za kuweko madarakani mara chungu nzima imekosoa utendaji dhidi ya Uzayuni ndani ya Umoja wa Mataifa na kwa sababu hiyo ndio maana imejitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Mara hii pia, kisingizio cha serikali ya Trump cha kupinga bajeti ya Umoja wa Mataifa ni kutengwa fedha maalumu kwa ajili ya hafla ya kumbukumbu ya mkutano wa kupinga ubaguzi wa Durban Afrika Kusini uliofanyika mwaka 2001. Mkutano wa Kimataifa wa Kupinga Ubaguzi wa Durban, Afrika Kusini ulikosoa vikali ubaguzi unaofanywa na utawala haramu wa Israel. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, baada ya kupita miaka 20, tangazo la Durban sio kitu cha kufanyia sherehe au kuidhinisha hilo.

 

Kwa muktadha huo, serikali ya Trump kama inavyodhani, inafanya juhudi ili kuufanya Umoja wa Mataifa ubadilishe misimamo yake ya sasa katika kulaani hatua za kijinai za Israel na vile vile kulaani Uzayuni kama aina ya ubaguzi.

Jambo la pili lililoifanya Marekani kupinga kupasishwa bajeti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa ni kuwa, asasi hiyo ya kimataifa imekataa kuwa pamoja na serikali ya Trump katika uga wa kushadidisha mashinikizo na vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa msingi huo, serikali ya Trump ikiwa katika dakika za lala salama za uhai wake wa kisiasa, imeshindwa na kupata pigo jingine. Katika mchakato wa upigaji kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jumatano iliyopita,  uliofanyika kwa minajili ya kuunda tena kamati ya vikwazo na kamati ya kitaalamu ili kutekelea upya vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran ambalo limekuwa takwa la kukaririwa la Marekani, siyo nchi washindani na wapinzani tu wa Washington zilizolipinga dola hilo la kibeberu  bali hata washirika wake wa Ulaya.

Mkutano wa Kimataifa wa Kupinga Ubaguzi wa Durban Afrika Kusini uliofanyika mwaka 2001

 

Ni idadi ndogo mno ya nchi waitifaki wa Marekani ndizo zilizokuwa pamoja na takwa hilo la Washington, kwani nchi 110 zilipiga kura ya kupinga takwa hilo la Marekani. Aidha nchi 32 zilijizuia kupiga kura huku mataifa 10 tu yakiamua kuwa pamoja na Marekani. Kwa muktadha huo, serikali ya Trump imepata pigo jingine katika siku zake za mwisho mwisho za kuweko uongozini.

Septemba 20 mwaka uliopita, serikali ya Trump ilidai kwamba, imezindua mchakato wa kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Hata hivyo, uamuzi huo ulikabiliwa na upinzai wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Licha ya hayo, lakini Marekani ikang’ang’ania msimamo wake kwamba, imehuisha vikwazo dhidi ya Iran na ni kwa sababu hiyo ndio maana inataka kuundwa tena kamati ya vikwazo.

Uzayuni ni ubaguzi

 

Nathalie Tocci, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na mahusiano ya kimataifa wa Italia na ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Mahusiano ya Kimataifa cha Italia  anasema kuwa, matokeo ya hivi karibuni ya kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kupinga pendekezo la Marekani  la kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran lilikuwa pigo kubwa mno kwa diplomasia ya serikali ya Trump.

Inavyoonekna ni kuwa, Marekani huridhishwa na Umoja wa Mataifa na utendaji wake pale tu asasi hiyo inapofanya mambo kwa maslahi na matakwa ya taifa hilo. Hivi sasa pia ambapo Umoja wa Mataifa na akthari ya wanachama wake hawakubaliani na matakwa ya serikali ya Trump, unakabiliwa na vizingiti vya Washington katika mchakato wa upasishaji bajeti ya kila mwaka ya umoja huo, ili kwa njia hiyo kuandaliwe uwanja na serikali ya Washington wa kuishinikiza taasisi kubwa zaidi ya kimataifa.

Tags