Jun 02, 2024 06:37 UTC
  • Kiwanda cha Dangote chaanza kuuzia Ulaya mafuta ya ndege

Kiwanda cha Kusafishia Mafuta cha Dangote cha Nigeria kimeanza kuziuzia nchi za Ulaya mafuta ya ndege.

Vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti jana Jumamosi kuwa, tani 45,000 za mafuta ya ndege zinasafirishwa kwa meli ya Doric Breeze na Shirika la Petroli la Uingereza BP kutoka Kiwanda cha Kusafishia Mafuta cha Dangote jijini Lagos, kuelekea mjini Rotterdam nchini Uholanzi.

Kiwanda hicho ambacho ni kikubwa zaidi barani Afrika, kilizinduliwa rasmi Mei 2023, lakini kilianza uzalishaji wa dizeli na mafuta ya usafiri wa anga Januari mwaka huu, na hivyo kuashiria hatua kubwa katika shughuli zake na sekta ya petroli ya Nigeria kwa ujumla.

Mradi wa Kusafisha Mafuta na Petrokemikali wa Dangote, uliopo Eneo Huru la Kiviwanda na Kibiashara la Dangote jijini Lagos, una uwezo wa kusafisha mapipa 650,000 ya mafuta ghafi kwa siku. Kiwanda hicho cha kusafisha mafuta kimejengwa katika eneo la takriban hekta 2,635.

Kiwanda cha Dangote

Kuna matumaini miongoni mwa Wanigeria kwamba kiwanda hicho kitachangia kupunguza bei ya bidhaa za petroli na uwezekano wa kubadlisha sekta ya nishati ya nchi hiyo katika miaka ijayo.

Ingawa Nigeria ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika na pia ina uchumi mkubwa zaidi barani humo, lakini nchi hiyo kwa sasa inategemea pakubwa mafuta na dizeli kutoka nje kwa sababu ya ukosefu wa uwezo wa kusafisha.

Tags