Mikakati athirifu ya Iran ya kutatua migogoro ya kikanda na Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i112490-mikakati_athirifu_ya_iran_ya_kutatua_migogoro_ya_kikanda_na_palestina
Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na mikakati madhubuti na athirifu katika matukio ya kieneo na kimataifa ikiwemo kadhia ya Palestina.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jun 02, 2024 23:30 UTC
  • Mikakati athirifu ya Iran ya kutatua migogoro ya kikanda na Palestina

Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na mikakati madhubuti na athirifu katika matukio ya kieneo na kimataifa ikiwemo kadhia ya Palestina.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa na nafasi chanya na athirifu katika matukio ya kieneo na ya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni. Kuzingatia umuhimu wa uhusiano na ushirikiano wa kieneo, na kuzuia uingiliaji wa kigeni imekuwa moja ya misingi isiyobadilika na imara ya siasa za nje za Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mstari wa mbele katika kupanua ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni pamoja na usalama na majirani zake na inaona kuwa, njia pekee ya kudumisha amani na usalama katika eneo ni kuzuia uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya eneo hili na mataifa yote kuwa na ushiriki katika hilo.

Matukio ya Palestina ni sehemu muhimu ya sera za kigeni za Iran na viongozi wa Iran daima wamekuwa wakisisitiza kuwa, njia pekee ya kuondokana na migogoro ya kieneo ikiwemo kadhia ya Palestina ni kutafuta suluhu na utatuzi madhubuti na endelevu kwa Wapalestina na eneo hili kwa ujumla.

Vita vya Gaza na jinai za utawala wa Kizayuni za kuwaua wanawake na watoto wa Kipalestina ziliweka wazi na bayana misimamo na siasa za Iran kuhusiana na Palestina. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza juu ya kufanyika kura ya maoni kwa kuwashirikisha wakaazi wote wa ardhi hiyo inayokaliwa kwa mabavu wakiwemo Wapalestina waliokimbia makazi yao. Kwa kufanya kura hiyo ya maoni, wamiliki halisi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu watangaze maoni na matakwa yao kuhusu hatima ya Palestina.

Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran

 

Katika barua yake kwa wanachuo wa vyuo vikuu vya Marekani kufuatia utetezi wao wa kijasiri kwa maslahi ya watu wa Palestina, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema:

Palestina ni nchi huru ya taifa linaloundwa na Waislamu, Wakristo na Wayahudi ambayo ina historia ndefu sana. Baada ya Vita vya Dunia, mabepari wa mtandao wa Kizayuni, wakisaidiwa na serikali ya Uingereza, hatua kwa hatua walituma magaidi elfu kadhaa katika ardhi hii; wakavamia miji na vijiji vyake, ambapo waliua kwa umati maelfu ya watu au kuwafukuza na kuwahamishia katika nchi jirani. Walipora na kunyakua nyumba, masoko, na mashamba yao, na wakaanzisha taifa linaloitwa Israeli katika ardhi iliyonyakuliwa ya Palestina.

Ayatullah Khamenei anasema katika sehemu nyingine ya barua yake hiyo: Muungaji mkono mkuu wa utawala huu ghasibu, baada ya misaada ya kwanza ya Uingereza, ni serikali ya Marekani, ambayo imeendeleza uungaji mkono wake wa kisiasa, kiuchumi na silaha kwa utawala huo, na hata kufanya uzembe usiosameheka kwa kuufungulia njia ya kuzalisha silaha za nyuklia, na kuusaidia katika njia hiyo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sanjari na misimamo yake yenye misingi mikuu ya kutetea haki halali za wananchi wa Palestina pia imeongeza ushirikiano na mashauriano na nchi ziingine za eneo na ulimwengu wa Kiislamu.

Imamu Khomeini alitoa umuhimu mkubwa kwa suala la Palestina na aliitangaza Ijumaa ya mwiisho ya mwezi wa Ramadhani kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya Quds

 

Ali Bagheri Kani; Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Ahmed Attaf, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Algeria kuhusiana na matukio ya hivi punde ya vita vya Gaza na jinai za utawala wa Kizayuni na kusisitiza juu ya umuhimu wa kuchukuliwa hatua za dharura na za pamoja za nchi za Kiislamu kwa ajili ya kusimamisha jinai za utawala ghasibu dhidi ya watu wa Palestina na kuongeza misaada kwa Gaza. Aidha ametangaza pendekezo la Iran la kufanyika mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Ukweli wa mambo ni kuwa, matukio ya eneo baada ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa yamedhihirisha kuliko wakati mwingine wowote ule juu ya kuwa katika haki Iran na utendaji wake athirifu katika  kutatua mgogoro wa Palestina.  Utendaji wa daima wa Iran katika kukabiliana na uingiliaji wa kigeni, umuhimu wa ushirikiano wa kieneo na utumiaji wa uwezo wa Ulimwengu wa Kiislamu, ni miongoni mwa mambo athirifu ambayo yatasambaratisha njama na malengo maovu ya maajinabi na mkabala wake, kuandaa mazingira ya kisiasa kwa ajili ya kuleta utulivu na usalama katika eneo hili kwa kutanguliza mbele suala la utatuzi wa mgogoro wa Palestina.