Usajili wa wanaotaka kugombea urais Iran wamalizika, kampeni kuanza Juni 12
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i112516-usajili_wa_wanaotaka_kugombea_urais_iran_wamalizika_kampeni_kuanza_juni_12
Shughuli ya kujiandikisha viongozi wanaotaka kugombea uchaguzi wa mapema wa duru ya 14 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu inamalizika jioni ya leo Juni 3.
(last modified 2024-06-03T08:00:21+00:00 )
Jun 03, 2024 08:00 UTC
  • Usajili wa wanaotaka kugombea urais Iran wamalizika, kampeni kuanza Juni 12

Shughuli ya kujiandikisha viongozi wanaotaka kugombea uchaguzi wa mapema wa duru ya 14 ya urais wa Jamhuri ya Kiislamu inamalizika jioni ya leo Juni 3.

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Es’haq Jahangiri, ni miongoni mwa shakhsia watajika waliofika katika Makao Makuu ya Uchaguzi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran hapa Tehran kwa ajili ya kujiandikisha.

Kadhika, wabunge kadhaa wa zamani wakiwemo Elias Naderan, Hassan Sobhani, Hassan Kamran Dastjerdi, na Vahid Jalalzadeh wamejiandikisha kuwania kiti hicho hii leo, ikiwa ni siku ya tano na ya mwisho ya usajili huo.

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Es’haq Jahangiri,

Hadi sasa idadi ya watu waliojiandikisha kugombea kiti cha rais nchini Iran imepindukia 20 kati ya watu 80 waliokuwa na azma hiyo, baada ya viongozi zaidi kujiandikisha kuwania nafasi hiyo leo Jumatatu.

Jana Jumapili, Mahmoud Ahmadinejad, rais wa zamani wa Iran alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri waliojiandikisha kugombea urais. Aliongoza Iran kwa awamu mbili mfululizo, baina ya mwaka 2005 na 2013.

Mahmoud Ahmadinejad, rais wa zamani wa Iran akihutubia wanahabari baada ya kujiandikisha

Mbunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Zohreh Elahian siku ya Jumamosi alikuwa mwanamke wa kwanza kujiandikisha kugombea uchaguzi wa rais 2024.

Watu wote waliojiandikisha kuwania urais, sharti wapigwe msasa na Baraza la Kulinda Katiba la Iran lenye wanachama 12, kabla ya kuidhinishwa kugombea nafasi hiyo, iliyobaki wazi baada ya kufa shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta Mei 19.

Mbunge Zohreh Elahian

Orodha ya mwisho ya watakaoidhinishwa kuwania urais itatangazwa Juni 11, siku moja kabla ya kuanza rasmi kampeni za uchaguzi, zitakazoendelea hadi Juni 26. Uchaguzi wa mapema wa kuwania urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umepangwa kufanyika Ijumaa ya Juni 28