Adam Schiff ataka kutolewa ripoti kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i66040-adam_schiff_ataka_kutolewa_ripoti_kuhusu_mauaji_ya_jamal_khashoggi
Mkuu wa Kamati ya Intelijinsia katika Bunge la Wawakilishi la Marekani amemwandikia barua Mkuu Mpya wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo akitaka kutolewa ripoti kuhusu mauaji ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 24, 2021 04:35 UTC
  • Adam Schiff ataka kutolewa ripoti kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi

Mkuu wa Kamati ya Intelijinsia katika Bunge la Wawakilishi la Marekani amemwandikia barua Mkuu Mpya wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo akitaka kutolewa ripoti kuhusu mauaji ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia.

Adam Schiff amemwandikia barua Aurel Hines Mkuu Mpya wa Usalama wa Taifa wa Marekani na kutaka kubainishwa kikamilifu ripoti  kuhusu mauaji ya Khashoggi mwandishi habari mtajika aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud. 

Adam Schiff, Mkuu wa Kamati ya Intelijinsia katika Bunge la Wawakilishi la Marekani

Katika barua hiyo Schiff ametaka kutolewa ripoti itakayokuwa na ushahidi kuhusu taarifa na kuhusika kila afisa wa sasa na wa zamani wa Saudi Arabia au shakhia yoyote wa kisiasa wa sasa au wa zamani wa nchi hiyo katika kuongoza, kuamuru au kuwepo nyaraka au ushahidi wowote wa kuhusika kwao katika mauaji ya Khashoggi. 

Jamal Khashoggi aliuawa kikatili na kisha mwili wake kukatwa vipande vipande tarehe Pili mwezi Oktoba mwaka 2018 baada ya kuingia ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul Uturuki. 

Saudi Arabia ilikaa kimya kwa siku 18 bila ya kusema lolote baada ya kujiri mauaji hayo ya kutisha hadi pale serikali ya Uturuki ilipotoa ripoti mbalimbali na Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilipothibitisha kuwa Khashoggi aliuawa kwa amri ya moja kwa moja kutoka kwa Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.