Mar 16, 2021 02:37 UTC
  • Indhari kuhusu ubaguzi katika utoaji chanjo ya COVID-19 duniani

Ingawa kugunduliwa chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 au corona ni jambo ambalo liliibua matumaini duniani kote, lakini ugavi usio wa kiudilifu wala usawa wa chanjo hiyo ni jambo ambalo limewakasirisha wengi na hata kuibua kelele katika baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya. Kuhusiana na nukta hiyo Kansela Sebastian Kurz wa Austira amesema hakuna uadilifu katika usambazwaji chanjo ya COVID-19 barani Ulaya.

Ameongeza kuwa: "Baadhi ya wanachama wa Umoja wa Ulaya wamepata kiwango kikubwa cha dozi za COVID-19 ikilinganishwa na nchi zingine. Bado madola makubwa ya Ulaya yanazuia usambazwaji chanjo ya COVID-19 katika Umoja wa Ulaya. Katika hali ambayo usambazwaji chanjo ya COVID-19 ni jambo ambalo linapaswa kuangaziwa kwa mtazamo wa ubinadamu na hivyo ni wajibu wa madola yenye nguvu na yenye utajiri mkubwa duniani kusaidia chanjo hiyo kufika kote duniani, lakini hivi sasa tunashuhudia namna ambavyo madola makubwa katika Umoja wa Ulaya yanazuia chanjo hiyo kuenezwa kwa usawa hata katika nchi za umoja huo.

Uhaba wa chanjo ya corona na kuchelewa shirika la Uswisi-Uingereza la  AstraZeneca katika kukidhi mahitaji ya chanjo ya Umoja wa Ulaya, ukosefu wa stratijia ya pamoja katika umoja huo na kutowekwa sera ya kugawa kwa uadilifu chanjo miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ni jambo ambalo limepelekea nchi nyingi za Ulaya kukosoa utendaji kazi wa umoja huo.

Hivi sasa, kutokana na kuendelea janga la COVID-19 na kuibuka aina mpya ya kirusi hicho barani humo ambacho sasa kimeenea maeneo mengine duniani, hitilafu kuhusu usambazwaji chanjo zimezidi kuongezeka baina ya nchi za Umoja wa Ulaya. Nchi kama vile Denmark,  Jamhuri ya Czech,  Austria, Hungary, na Slovakia zinasema Umoja wa Ulaya umegueza kadhia ya chanjo ya corona kuwa kadhia ya kisiasa. Hivi sasa nchi hizo zimeamua kununua chanjo ya corona kutoka nje ya Umoja wa Ulaya. Hayo yanajiri katika hali ambayo wakuu wa Umoja wa Ulaya wanazozana na Marekani na Uingereza kuhusu ununuzi wa chanjo ya corona.

Aidha kuna hitilafu baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya baada ya shirika la Uswisi-Uingereza la  AstraZeneca kutangaza kuwa haliko tayari kupunguza mauzo yake kwingineko duniani ili kukidhi mahitaji ya Umoja wa Ulaya.

Charles Michel, mwenyekiti wa Baraza la Ulaya anasema hivi kuhusu nukta hii: "Ikiwezekana tutatumia uwezo wote wa kisheria na amri za kiserikali ili kuhakikisha kuwa tunakidhi mahitaji ya chanjo ya watu wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya umelitisha shirika la AstraZeneca kuwa iwapo halitafungamana na ahadi zake basi halitaruhusiwa kuuza nje chanjo ambayo imetengenezwa ndani ya  Ulaya.  Kwa msingi huo shehena iliyotengenezwa na shirika hilo nchini Uingereza imezuiwa kuuzwa Australia.

Hivi sasa vita vya ugavi wa chanjo ya corona vimeshadidi na hata Marekani nayo imepiga marufuku uuzaji nje chanjo ya corona.

Raia wa Uganda akipata chanjo ya corona

Kutokana na hali hiyo imedokezwa kuwa hivi sasa chanjo ya corona inauzwa kimagendo na kuna mikataba ya siri baina ya mashirika ya kutengeneza chanjo na baadhi ya nchi zinazohitaji chanjo hiyo. Kadhia hii ya chanjo ya corona imewakasirisha wengi ambao wanasema ubinadamu  hauzingatiwi. Kati ya wakosoaji wakubwa ni Kansela wa Austira ambaye amezituhumu baadhi ya nchi za Ulaya kuwa zimetia saini mapatano ya siri ya kununua chanjo ya corona.

Haya yanajiri wakati ambao mashirika ya kimataifa yanasisitiza kuwa chanjo ya corona inapaswa kusambazwa kwa usawa kote duniani na bila ya kutumia vigezo vya kisiasa. Inavyoelekea ni kuwa hivi sasa nchi za Ulaya na Marekani zinatekeleza sera za ubaguzi wa rangi sawa na ule wa mfumo wa Apartheid katika usambazaji chanjo ya COVID-19 duniani.

Tags