Mataifa ya Kiislamu yatakiwa kulipa uzito suala la ukombozi wa Quds
(last modified Wed, 05 May 2021 06:30:28 GMT )
May 05, 2021 06:30 UTC
  • Mataifa ya Kiislamu yatakiwa kulipa uzito suala la ukombozi wa Quds

Mwanaharakati mmoja nchini Russia ametoa mwito kwa mataifa ya Kiislamu kulipa kipaumbele cha kwanza suala la ukombozi wa Quds tukufu na kadhia ya Palestina kwa ujumla.

Emil Ashurov, mwanaharakati Muislamu wa Russia ambaye pia ni mwanachama wa Jumuiya ya Kulihami Taifa la Palestina alitoa mwito huo jana Jumanne katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, Quds tukufu inaweza kukombolewa tu kupitia mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu.

Amewaasa Waislamu kufuata miongozo ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ili waweza kufanikisha ndoto za kuikomoa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Mwanaharakati huyo wa Russia ameyataka mataifa ya Kiislamu kutoruhusu wanasiasa kufuatilia sera zao za usaliti kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Siku ya Kimataifa ya Quds huadhimishwa katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kila mwaka

Amesema, "al-Quds inayokaliwa kwa mabavu na Uzayuni wa kimataifa, ndio moyo wa ulimwengu wa Kiislamu, na hivyo kadhia ya Palestina ni muhimu mno kwa Waislamu wote duniani.

Kadhalika Emil Ashurov anasisitiza kuwa, 'Muamala wa Karne' ambao ulipendekezwa na utawala uliopita wa Marekani wa Donald Trump ulibuniwa kwa shabaha ya kutaka kupuuzwa haki za Wapalestina, lakini mpango huo utasambaratika kutokana na umoja wa umma wa Kiislamu.