China: Marekani inahatarisha amani kwenye langobahari la Taiwan, mapigano yanaweza kutokea
China imekosoa harakati za kichochezi zinazofanywa na Marekani katika langobahari la Taiwan na kueleza kwamba, kuweko manowari ya Marekani katika eneo hilo kunahatarisha amani na uthabiti katika njia hiyo ya baharini ya maji ya kimataifa.
Taarifa iliyotolewa mapema leo na Kamandi ya Kijeshi ya Mashariki ya China imeeleza kuwa, hatua ya Marekani ya kuptisha manowari yake katika langobahari hasasi la Taiwan linalokitenganisha kisiwa hicho na China itasababisha mivutano na kuvuruga shughuli za biashara za kimataifa na kwamba ni jukumu la Beijing kufuatilia harakati za meli zinazopita katika langobahari hilo.
Taarifa hiyo ya serikali ya China imesisitiza pia kuwa, uingiliaji wowote wa kigeni katika langobahari la Taiwan unaweza kusababisha mapigano katika eneo hilo.
Kitengo cha saba cha jeshi la majini la Marekani kimetangaza kuwa manowari yake ya kuangamiza makombora ya USS Curtis Wilbur jana Jumanne ilipita kwenye langobahari la Taiwan, katika kile ilichodai kuwa ni "safari za kawaida katika langobahari la Taiwan" zinazofanywa kulingana na sheria za kimataifa.

Marekani ina imani kwamba, ili kuizuia China isigeuke kuwa dola kuu la kikanda, inapasa kuidhibiti nchi hiuyo kwa kutekeleza sera zile zile ilizotumia dhidi ya lililokuwa Shirikisho la Kisovieti la Urusi ya zamani.
Hata hivyo serikali ya Beijing imetangaza mara kadhaa kuwa, kinyume na inavyoeleza Marekani, China haiko tayari kuyatoa mhanga maslahi yake ya kitaifa kwa uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na itatoa jibu kali bila kujali chochote kwa vitisho vyovyote vitakavyokuwa hatarishi kwa nchi hiyo. Aidha China haikubaliani na harakati za kutaka kujitawala zinazofanywa na Taiwan, ikisisitiza kuwa kisiwa hicho kitabaki kuwa eneo lisilotenganika na ardhi ya nchi hiyo.../