50 wapoteza maisha katika ajali ya ndege ya kijeshi Ufilipino
https://parstoday.ir/sw/news/world-i71998
Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha huku wengine wasiopungua 49 wakijeruhiwa, baada ya ndege ya kijeshi ya Ufilipino kuanguka na kuteketea moto kusini mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 05, 2021 02:48 UTC
  • 50 wapoteza maisha katika ajali ya ndege ya kijeshi Ufilipino

Kwa akali watu 50 wamepoteza maisha huku wengine wasiopungua 49 wakijeruhiwa, baada ya ndege ya kijeshi ya Ufilipino kuanguka na kuteketea moto kusini mwa nchi.

Ndege hiyo ya kijeshi ya C-130 Hercules iliyokuwa imebeba watu 100, aghalabu yao wakiwa makurutu wa kijeshi waliofuzu hivi karibuni, ilianguka ilipokuwa ikijaribu kutua katika Kisiwa cha Jolo katika mkoa wa Sulu wa kusini mwa nchi.

Meja Jenerali William Gonzales, Kamanda wa Kikosi cha Pamoja katika mkoa wa Sulu amesema katika taarifa kuwa, baadhi ya wanajeshi waliruka kutoka kwenye ndege hiyo kabla ya kudondoka na kuwaka moto. Amesema hii ni moja ya ajali mbaya zaidi kuwahi kukikumba kikosi cha anga cha jeshi la nchi hiyo.

Kanali ya Pondohan TV ya nchi hiyo imetangaza kuwa, hatima ya abiria 17 waliokuwemo kwenye ndege hiyo haijajulikana, hadi wakati tunamaliza kuandaa taarifa hii.

Ndege nyingine ya kijeshi ya Hercules ( iliyotengenezewa US) iliyoanguka na kuwaka moto Indonesia 

Jenerali Cirilito Sobejana, Mkuu wa Majeshi ya Ufilipino amesema ndege hiyo ya kijeshi ilikuwa imewabeba askari kutoka katika eneo la Cagayan de Oro kwenye kisiwa cha kusini cha Mindanao, na ilishindwa kutua katika barabara yake maalumu, na ndipo ikaanguka na kuwaka moto.

Kwa upande wake, Seneta Richard Gordon ameeleza wasi wasi kuwa, huenda nchi hiyo inanua ndege mbovu kutoka Marekani, kwani hii ni ajali ya nne ya ndege ya kijeshi kutokea nchini humo mwaka huu pekee.