Kongresi ya Marekani yaishinikiza EU iitambue Hizbullah kama kundi la kigaidi
(last modified Wed, 28 Jul 2021 07:17:51 GMT )
Jul 28, 2021 07:17 UTC
  • Kongresi ya Marekani yaishinikiza EU iitambue Hizbullah kama kundi la kigaidi

Kundi moja la wawakilishi wa vyama viwili vya Republican na Democratic katika Kongeresi ya Marekani limetoa wito wa kushinikizwa Umoja wa Ulaya ili uitambua harakati yote ya Hizbullah kuwa ni "kundi la kigaidi".

Wawakilishi 10 kutoka vyama hivyo viwili wamewasilisha muswada katika Kongresi ya Marekani wakitaka kushinikizwa Umoja wa Ulaya ili utengua hatua yake ya kutofautisha baina ya kazi za kisiasa za chama cha Hizbullah ya Lebanon na zile za kijeshi za harakati hiyo ya mapambano.

Marekani imeiweka Hizbullah ya Lebanon katika orodha yake ya eti makundi ya kigaidi.

Hata hivyo Umoja wa Ulaya, tofauti na Marekani, umetofautisha baina na harakati za kisiasa za Hizbullah na tawi la kijeshi la kundi hilo na kuliweka tawi lake la kijeshi katika orodha ya makundi eti ya kigaidi yaliyowekewa vikwazo ya umoja huo.

Baada ya mafanikio makubwa ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi yanayofadhiliwa na nchi za Magharibi na vibaraka wao wa Kiarabu, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zimezidisha kampeni ya kuibana na kuzidisha mashinikizo dhidi harakati hiyo ya mapambano.

Katika mkondo huo Marekani imeziwekea vikwazo benki na viongozi kadhaa wa Lebanon kwa kisingizio kwamba wanashirikiana na Hizbullah.