Watu 1000 wameuawa Myanmar tangu yajiri mapinduzi ya kijeshi
(last modified Wed, 18 Aug 2021 16:26:30 GMT )
Aug 18, 2021 16:26 UTC
  • Watu 1000 wameuawa Myanmar tangu yajiri mapinduzi ya kijeshi

Makundi ya wanaharakati nchini Myanmar yamesema watu zaidi ya elfu moja wameuawa tangu yalipojiri mapinduzi ya kijeshi nchini humo mwezi Februari mwaka huu.

Tate Naing, Katibu wa chama kinachopigania maslahi ya wafungwa wa kisiasa cha Assistance Association for Political Prisoners (AAPP) ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: Watu 1,001 wasio na hatia wameuawa tokea Februari mwaka huu.

Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka huu baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.

Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai ya kutokea wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana ambapo chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.

Maandamano ya ghasia ya kupinga utawala wa kijeshi Myanmar

Katibu wa chama cha AAPP amebainisha kuwa, idadi halisi ya waliouawa ni kubwa zaidi, na kwamba jeshi limekataa kuwapa takwimu za raia waliouawa, na linasisitiza kuwa askari wake kadhaa wameuawa pia katika ghasia hizo za baada ya mapinduzi.

Mapema mwezi huu, Balozi na mwakilishi wa Myanmar katika Umoja wa Mataifa alisema kuwa, jeshi la Myanmar lililotwaa madaraka ya nchi kwa nguvu limefanya mauaji ya umati nchini humo. Kyaw Moe Tun ambaye amekataa kuachia nafasi hivyo licha ya kutimuliwa baada ya jeshi kutwaa madaraka nchini Myanmar amesisitiza kuwa, kwa akali watu 40 waliuawa kwa umati wakiwemo watoto mwezi uliopita wa Julai katika eneo la Sagaing.