Mar 06, 2022 04:49 UTC
  • Russia yaonya kuhusu kutumwa magaidi wa ISIS nchini Ukraine

Idara ya Ujasusi wa Nje ya Russia (SVR) imesema katika taarifa yake ya siku ya Ijumaa kwamba Marekani inawapa mafunzo magaidi wa Daesh (ISIS) katika kituo cha Al-Tanf nchini Syria ili wapelekwe Ukraine.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kambi ya al-Tanf inayodhibitiwa na Marekani nchini Syria inatumiwa kwa ajili ya maandalizi na kutoa mafunzo kwa magaidi wa Daesh ili kutumwa Ukraine na kutumiwa mashariki mwa nchi hiyo huko Donbas.

Idara ya Ujasusi ya Nje ya Nchi ya Russia imesema: "Mwishoni mwa mwaka 2021, Wamarekani waliwaachilia huru makumi ya magaidi wa ISIS raia wa Russia na jamhuri zinazojitawala za Urusi ya zamani na kuwapeleka katika kambi ya Al-Tanf inayodhibitiwa na Marekani, ambako wanapewa mafunzo ya kutekeleza operesheni maalumu, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kufanya uharibifu na hujuma za kigaidi katika eneo la Donbas."

Taarifa ya SVR imeongeza: Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Kamandi ya Operesheni Maalumu ya Marekani inaendelea kuunda vitengo vipya vya Daesh Magharibi mwa Asia na nchi za Afrika na imepangwa kuwa, magaidi hao watapelekwa Ukraine kwa kushirikiana na mashirika ya ujasusi ya nchi wanachama wa shirika la NATO. Marekani imepanga kuwatumia magaidi hao wa Daesh katika kazi za uharibifu na hujuma za kigaidi dhidi ya Russia nchini Ukraine kupitia ardhi ya Poland. 

Onyo la Russia kuhusu harakati za Marekani za kuwapa mafunzo na kuwasafirisha magaidi wa kitakfiri wakiwemo wa Daesh kutoka Syria na kwingineko hadi Ukraine, linaonyesha kuwa, Washington inaendeleza siasa zake za awali za kuwatumia magaidi kwa ajili ya kutimiza malengo yake makuu. 

Marekani imekuwa ikitekeleza siasa za kuyaunga mkono moja kwa moja na kuyapa silaha makundi ya kigaidi nchini Syria baada ya machafuko ya mwaka 2011 kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya nchi hiyo na kudhoofisha mhimili wa muqawama. Washington pia imekuwa ikitumia sera na siasa hizo huko Iraq, na wapiganaji wa harakati ya wananchi ya al Hashdul Shaabi wamekuwa wakionya mara kwa mara juu ya uungaji mkono wa Marekani kwa Daesh na kuwapeleka katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wa Afghanistan, Marekani pia ilifuata mtindo huo kabla ya kuondoka nchini humo, ikiwaunga mkono na kuwasaidia magaidi wa Daesh kufanya mashambulizi na hujuma za kigaidi katika nchi hasimu na wapinzani wake, jirani na Afghanistan. Kwa hakika sera ya jumla ya Marekani ni kuwatumia magaidi kuwashambulia maadui zake.

Hivi sasa suala hili linafanyika kwa mara ya kwanza katika bara la Ulaya kwa kuwatuma mashariki mwa Ukraine magaidi wa Daesh waliopewa mafunzo kwenye kambi ya Al-Tanf ili kupigana na vikosi vya jeshi la Russia na wanamgambo wa maeneo ya Donetsk na Luhansk.

Inatupasa kusema hapa kuwa, Marekani haiko peke yake katika suala hili, kwani Uturuki, mwanachama mwingine wa NATO ambaye amepata uzoefu sawa na kutuma magaidi wa kitakfiri huko Libya na Nagorno-Karabakh, pia inataka kutuma magaidi huko Ukraine.

Tarehe 2 mwezi huu wa Machi, Saeed Fars al-Saeed, mchambuzi wa Kisyria wa masuala ya kistratijia alitangaza kuwa, mamia ya magaidi wanajiandaa kuingia Ukraine chini ya mwamvuli wa Idara ya Ujasusi ya Uturuki (MIT). Fars al-Saeed amesema: "Magaidi 2,500 waliopo katika mkoa wa Idlib huko Syria wako tayari kushiriki katika vita dhidi ya Russia. Idara ya Ujasusi ya Uturuki inasimamia kazi ya kuwahamisha magaidi hao hadi Poland na kisha Ukraine, na wengi kati ya magaidi hao wana uraia wa Syria, nchi nyingine za Kiarabu au Chechnya. Uturuki ndio nchi bora kwa ajili ya kuwavusha salama magaidi kwenda Poland na kutoka huko hadi Ukraine kukabiliana na jeshi la Russia."

Hivyo, inaonekana kuwa Marekani na washirika wake ambao daima wamekuwa wakifuata sera za kindumakuwili kuhusu suala la ugaidi na kuyaimarisha makundi ya kigaidi kwa maslahi yao, sasa wanakusudia kufanya hivyo barani Ulaya, lakini mara hii dhidi ya Russia na waitifaki wake huko Ukraine. Tajriba ya huko nyuma na jinai za magaidi wa kitakfiri huko Syria na Iraq zinaonyesha kwamba Marekani na washirika wake hawazingatii kanuni zozote za kimaadili na kibinadamu katika vita hivyo, na tunapaswa kusubiri kukaririwa jinai zao nchini Ukraine.

Tags