Apr 18, 2022 11:13 UTC
  • Kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya na vigezo vya  undumakuwili kuhusu uhuru wa kujieleza

Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu na vitendo vya mabavu dhidi ya Waislamu vimeongezeka katika miaka ya karibuni katika nchi za Ulaya. Kujitokeza na kuongezeka kwa harakati, vyama na watu wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia kumekuwa na nafasi kuu katika uwanja huo.

Tukio la karibuni kabisa la chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya, ni jitihada za mtu mmoja kutoka mrengo wa kulia mwenye chuki dhidi ya Uislamu huko Sweden za kuchoma moto Qur'ani Tukufu; kitendo ambacho kimeibua mapigano. Rasmus Paludan ambaye ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na kinachopinga Uislamu huko Denmark kwa jina la Hard Line pamoja na wafuasi wake walipanga kuandamana katika mji wa Linkoping  katika pwani ya mashariki mwa Sweden ili kukichoma moto kitabu cha Qur'ani Tukufu; hata hivyo kabla ya kuanza maandamano yao mapigano yalijiri kati ya polisi na Waislamu waliopinga kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu.   

Hii si mara ya kwanza kwa kundi hilo lenye misimamo ya kufurutu ada la mrengo wa kushoto kudhihirisha chuki dhidi ya Uislamu. Tarehe 28 Agosti mwaka 2020 pia mapigano kama hayo yalishuhudiwa katika mji wa Malmo huko Sweden na kusababisha ghasia za mitaani. Katika ghasia hizo, wafuasi wa kundi la Hard Line mbali na kupiga nara dhidi ya Uislamu walichoma moto nakala moja ya kitabu kitukufu cha Qu'rani; kitendo kilichokabiliwa na maandamano ya mamia ya Waislamu wa mji huo. Rasmus Paludan kiongozi wa chama cha Hard Line ambacho wanachama wake wana rekodi ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu huko Copenhagen mji mkuu wa Denmark wakati huo alisema kuwa wanafanya hivyo kwa lengo la eti kuwaamsha wananchi wa Sweden.   

Rasmus Paludan 

Serikali za Denmark na Sweden zinaliruhusu kundi hilo lenye misimamo mikali la mrengo wa kulia kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu na kuwadhalilisha Waislamu kwa kuchoma moto kitabu chao cha Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza na madai ya serikali hizo za Ulaya kuhusu kutetea uhuru huo wa kusema. Hata hivyo tunapotupia jicho vigezo vya undumakuwili vinavyotumiwa na nchi za Magharibi zikiwemo nchi za Ulaya kuhusu uhuru wa kujieleza tunaona kuwa uhuru wa kujieleza hutumiwa tu pale kadhia inayojadiliwa huwa ni kuivunjia heshima dini tukufu ya Uislamu na Waislamu; na kinyume chake masuala kama ngano ya Holocaust yaani madai ya kuuliwa Wayahudi katika Vita vya Pili vya Dunia au pale nchi fulani inapodhihirisha msimamo wa kuunga mkono maslahi ya Russia katika vita vinavyoendelea sasa huko Ukraine; serikali za Ulaya huonyesha radiamali kali dhidi ya shakhsia au nchi zinazoonekana kupingana mitazamo ya serikali hizo za Ulaya. 

Mfano wa wazi wa kitendo hicho cha kibaguzi na cha undumakuwili ni hatua ya jarida la Charlie Hebdo la nchini Ufaransa ya kuchapisha mara kwa mara vibonzo vinavyomdhalilisha na kumvunjia heshima Mtume Mtukufu wa Uislamu (S.A.W);  ambapo licha ya Waislamu nchini humo na katika nchi mbalimbali duniani kulalamika na kuandamana pakubwa kulaani kitendo hicho, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliunga mkono waziwazi kuchapishwa vibonzo hivyo vinavyomvunjia heshima Mtume Muhammad (S.A.W). Hatua ya Macron ya kutumia kisingizio cha uhuru wa kujieleza huko Ufaransa kwa ajili ya kuyavunjia heshima Matukufu ya Kiislamu kunakofanywa na jarida la Charlie Hebdo ilikosolewa vikali kimataifa na hata ndani ya Ufaransa kwenyewe. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa 

Katika upande mwingine, baada ya kufanyika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Rais wa Ufaransa na kisha kufuzu katika duru ya pili wagombea Emmanuel Macron mwenye misimamo inayodaiwa kuwa ya wastani  na Marine Le Pen mgombea mwenye siasa kali wa mrengo wa kulia, shakhsia hao wawili wamezidisha jitihada zao kwa kushadidisha misimamo yao ya chuki dhidi ya Uislamu ili kuvutia kura za wananchi wa Ufaransa. Marine Le Pen ambaye anapinga wahajiri na Uislamu amesema: Hijabu ni vazi la sare ambalo limekuwa likitumiwa na watu kwa muda sasa; vazi ambalo linadhihirisha misimamo mikali." Anaamini kuwa, kuvaa hijabu ya Kiislamu hadharani kunapaswa kutozwa faini, sawa kabisa na  makosa ya uendeshaji gari barabarani."

Marine Le Pen, mgombea wa kiti cha urais Ufaransa mwenye misimamo mikali 

Japokuwa Macron kidhahiri anaonekana kujiweka mbali na msimamo wa Le Pen kuhusu hijabu huku akidai kuwa hatabadili sheria yoyote lakini wakati huo huo tayari ameunga mkono sheria inayopiga marufuku vazi la hijabu mashuleni nchini Ufaransa. Kwa utaratibu huo, ni dhahir shahir kuwa, hakuna tofauti kati ya wanasiasa na serikali za Ulaya katika kuupinga Uislamu na kuwazidishia mbinyo na vizuizi mbalimbali Waislamu katika nchi za Ulaya. 

 

Tags