UN yataka kuchunguzwa ukatili wa Wazayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa
Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka na wa wazi kuhusiana na mashambulio ya kikatili ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya waumini wa Kipalestina waliokuwa wakifanya ibada katika Msikiti wa Al-Aqsa.
Wanajeshi wa Israel, wakishirikiana na walowezi wa Kiyahudi wameua shahidi, kujeruhi na kuwaweka kizuizini mamia ya Wapalestina na Waislamu katika kipindi cha wiki tatu zilizopita tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, na wamezidisha jinai zao na mashambulizi dhidi ya Msikiti wa Al-Aqswa na kuyavunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu.
Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) amesema katika mkutano mjini Geneva kwamba mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Wapalestina katika Msikiti wa Al-Aqsa huko Quds Mashariki (Jerusalem) yamejeruhi watu 180 wakiwemo watoto 27 kuanzia Aprili 15 hadi 17.aqsa

Msemaji wa OCHA ameongeza kuwa: "Lazima kufanyike uchunguzi wa haraka, usioegemea upande wowote, huru na wa wazi kuhusu mashambulizi ya askari wa Israel ambayo yamejeruhi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Al-Aqsa, na wale waliohusika lazima wawajibishwe."
Gazeti la al-Quds Al-Arabi pia limeandika leo Jumamosi kwamba Wapalestina 57 wamejeruhiwa katika mapigano kati ya wanajeshi wa Israel na waandamanaji wa Kipalestina katika viwanja vya Msikiti wa Al-Aqsa huko Quds Mashariki.
Ripoti zinasema makumi ya Wapalestina wamepigwa risasi na kujeruhiwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika mashafuko hayo.