Aug 24, 2022 04:18 UTC
  • Mgogoro wa nishati kuilazimisha Ulaya kutumia mkaa zaidi

Aghalabu ya nchi za Ulaya zitalazimika kutumia zaidi nishati ya mkaa katika msimu wa baridi kali unaolijongelea bara hilo, huku mgogoro wa nishati katika bara hilo ukishtadi.

Katibu Mkuu wa Shirika la Nishati ya Mkaa la Ulaya (Euracoal), Brian Ricketts amesema nchi nyingi za Ulaya kama Ujerumani, Ufaransa, Italia, Uhispania, Uholanzi, Austria, Poland, Hungary, Czech, Ugiriki na hata Uingereza zinatazamiwa kufufua kampuni zao za kuzalisha nishati ya mkaa.

Ricketts amesema, "Lengo la hatua tunazozichukua ni kuimarisha uthabiti (wa nishati) katika kipindi hiki kigumu."

Amesema bei ya mkaa kuanzia mwezi ujao wa Septemba itapindukia dola 405 kwa tani, kutoka dola 100 kwa tani katika kipindi kama hiki mwaka jana, na dola 60 mwaka juzi.

Ramani inayoonesha namna Ulaya inavyoitegeme Russia kwa nishati

Haya yanajiri huku mauzo ya gesi ya Russia kwa Ulaya yakipungua sana na kuziacha nchi nyingi za bara hilo zikikumbwa na tatizo la kujidhaminia nishati na kuongezeka gharama ya bidhaa hiyo muhimu.

Usambazaji wa gesi ya Russia kwenda Ulaya kupitia bomba la gesi la Nord Stream ulipungua kwa asilimia 60 hivi karibuni, na hivyo kusababisha bei ya gesi barani Ulaya kupanda sana. Hata hivyo, nchi za Ulaya bado zinaendelea kung'ang'ania sera yao ya vikwazo dhidi ya Russia, licha ya kuwa na madhara kwao pia. 

Tags