Sep 13, 2022 02:29 UTC
  • Taasisi ya utafiti: Uingereza inatunga sheria za kuwafanya Waislamu kuwa raia wa daraja la pili

Taasisi ya Mahusiano ya Mbari ya Uingereza (The Institute of Race Relations) imesema, sera ya serikali ya Uingereza inawafanya Waislamu wa nchi hiyo kuwa raia wa daraja la pili kutokana na sheria zinazoruhusu kupokonywa uraia wa Uingereza.

Gazeti la Uingereza la "The Guardian" limenukuu taasisi hiyo ikisema katika ripoti yake iliyotolewa Jumapili kwamba Sheria ya Utaifa na Ulinzi wa Mipaka, inayoruhusu kupokonywa uraia raia wanaostahili kupata uraia wa nchi nyingine, kimsingi inawalenga Waislamu, inaimarisha mizizi ya ubaguzi na kuunda uraia wa daraja ya chini kuliko ule wa Waingereza wengine.

Ripoti ya taasisi hiyo imesema kuwa, sera za serikali ya Uingereza kimsingi zinawalenga Waingereza wenye asili ya Asia Kusini, ambao wengi wao wanatoka katika jamii ya Kiislamu.

Gazeti hilo limemnukuu Frances Webber, makamu wa rais mtendaji wa taasisi hiyo akisema kwamba: "Ujumbe wa sheria hiyo inayohusiana na kupokonywa uraia tangu 2002 na utekelezaji wake, ambayo inatumiwa kwa kiasi kikubwa dhidi ya Waislamu wa Uingereza wenye asili ya Asia Kusini, ni kwamba hawa si raia halisi na hawatakuwa hivyo - licha ya kuwa na pasi za kusafiria za Uingereza -."

Weber ameongeza kuwa: "Ingawa raia wa Uingereza ambaye hana utaifa mwingine anaweza kufanya uhalifu mbaya zaidi bila kuhatarisha haki yake ya kubaki Muingereza, lakini hakuna raia wa Uingereza kati ya wale wanaoweza kupata uraia wa nchi nyingine, wanaokadiriwa kufikia milioni 6, anayeweza kujiamini kwamba atabakia na uraia wake."

Wakati huo huo maelfu ya watu wamefanya maandamano katika mji mkuu wa Uingereza, London kulaani mauaji ya mtu mmoja mwenye asili ya Afrika yaliyofanywa na askari polisi wa nchi hiyo.

Wamesikika wapiga nara za kulaani mauaji ya raia huyo mwenye asili ya Afrika aliyetambulika kwa jina la Chris Kaba. 

Ripoti ya vyombo vya habari inaonesha kuwa, mauaji ya watu weusi nchini Uingereza hivi sasa yameongezeka kwa kiwango cha kutisha tokea mwaka 2002. Raia 105 wenye asili ya Afrika waliuawa nchini humo mwaka 2020 pekee.

Tags