Kupungua thamani ya pauni; kudorora uchumi wa Uingereza
Ikiwa ni katika kuendelea kupanuka mgogoro wa kiuchumi barani Ulaya na athari za mpango wa kiuchumi wa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza Liz Truss, siku ya Ijumaa, thamani ya pauni ya nchi hiyo ilifikia kiwango chake cha chini kabisa katika kipindi cha miaka 37 iliyopita.
Pauni ya Uingereza ilishuka kwa asilimia 3 hadi chini ya dola 1.09 za Marekani na euro 1.12. Thamani ya sarafu hiyo katika soko la hisa la Uingereza pia ilipungua kutokana na mabadiliko makubwa ya sera za kiuchumi na kifedha za serikali mpya.
Uingereza imekuwa ikikabiliwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi katika mwaka mmoja uliopita. Ingawa nchi zote za Ulaya zinakabiliwa na matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la ugonjwa wa Covid-19 lakini Uingereza imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa zaidi kutokana na ukweli kwamba imekuwa ikikabiliwa na taathira za Brexit na kujitenga kwake rasmi na Jumuiya ya Ulaya. Matatizo hayo yameongezeka zaidi katika miezi ya karibuni kutokana na nafasi ya nchi hiyo katika vita vya Russia na Ukraine na msaada wake mkubwa wa kifedha na silaha kwa serikali ya Kiev; na hasa ikitiliwa maanani kwamba Russia imesimamisha usafirishaji wa gesi kwenda Ulaya.
Matokeo ya kupungua mauzo ya gesi ya Russia kwa Ulaya yameongeza gharama ya maisha kwa nchi za bara hilo, na nchi ambazo zilikuwa zikitegemea sana maliasili za Russia, ikiwemo Uingereza, zimeathirika zaidi na kupungua kwa mauzo hayo ya gesi. Kwa kadiri kwamba kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The Gurdian, ongezeko kubwa la bei ya nishati nchini Uingereza limeibua wasiwasi mkubwa nchini humo, hasa kwa wafanyabiashara na watumiaji. Maafisa wa nishati wa Uingereza wametangaza kuwa bei ya nishati itaongezeka kwa asilimia 80 mwezi Oktoba hadi wastani wa pauni 3,549 kwa mwaka, katika kile ambacho wataalamu wanasema ni mfano wa hivi karibuni wa matatizo ya ughali wa maisha katika nchi hiyo ya Ulaya.
Naeem Aslam, mtaalamu katika Taasisi ya Avatrade anasema kuhusu suala hilo kwamba: Wasiwasi juu ya kupanda gharama ya maisha nchini Uingereza umedhoofisha sana thamani ya pauni dhidi ya dola.
Kuongezeka pakubwa gharama ya maisha nchini Uingereza kumeiweka nchi hiyo katika hali mbaya zaidi ya kiuchumi katika nusu karne iliyopita. Hii ni katika hali ambayo, hakuna matarajio yoyote ya kuboreka hali hiyo, na maafisa rasmi wa nchi hiyo pia wanatahadharisha juu ya kuharibika zaidi hali ya mambo. Kwa mujibu wa ripoti zilizochapishwa kabla ya kuanza vita vya Russia na Ukraine, ilitabiriwa kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kingefikia asilimia 2 tu licha ya mashinikizo yaliyosababishwa na Brexit na janga la corona, lakini sasa kulingana na takwimu za Kituo cha Takwimu cha Kitaifa cha Uingereza, mfumuko wa bei tayari umefikia asilimia 10.1 na unatarajiwa kufikia asilimia 22 mwakani.
Gordon Brown, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Zaidi ya asilimia 70 ya Waingereza wanauchukulia umaskini, kutokuwepo usawa wa kijamii na mfumuko wa bei kuwa wasi wasi mkubwa zaidi unaowakabili maishani, na ikiwa mpango wa mabilioni ya pauni wa serikali mpya ya Uingereza hautatekelezwa vizuri, kuna uwezekano wa watoto wengine milioni 5 nchini kujiunga na safu ya watu maskini, na watu wengi zaidi nchini wataenda kwenye mabenki ya chakula ili kupokea mlo mmoja wa chakula cha msaada.
Serikali ya Uingereza imeahidi kubakisha gharama za nishati za familia katika kiwango cha pauni 2,500 kwa wastani katika kipindi cha miaka miwili ijayo, suala ambalo hata iwapo litafanikiwa halitatatua matatizo ya sehemu kubwa ya familia za Waingereza na hivyo kuzidisha tu pengo lililoko kati ya matabaka ya matajiri na maskini nchini. Hali hiyo imechochea malalamiko na ukosoaji wa kijamii nchini Uingereza.
Jarida la The Economist liliandika katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusiana na suala hilo kwamba: Hali ya kiuchumi nchini Uingereza ni mgogoro wa muda mrefu ambao umezidishwa na kujiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya. Uingereza sasa imenasa katika kinamasi cha miaka 15. Inataka kujionyesha kama soko lenye nguvu na huria, lakini wakati huo huo uchumi wake umebaki nyuma ya nchi nyingi tajiri duniani.