Oct 03, 2022 07:42 UTC
  • Uchaguzi wa rais Brazil waingia duru ya pili, Rais Bolsonaro kutoana kijasho na Lula da Silva

Uchaguzi wa rais wa Brazil umeingia duru ya pili baada ya wagombea kushindwa kupata nusu ya kura zote za wananchi katika kinyang'anyiro hicho kilichofanyika jana Jumapili.

Inácio Lula da Silva, mwanasiasa mkongwe wa Brazil mwenye umri wa miaka 76 na rais wa zamani wa nchi hiyo, amepata asilimia 47.9 ya kura (karibu kura milioni 55.5) na Jair Bolsonaro, rais wa sasa wa nchi hiyo, amepata asilimia 43.7 ya kura (karibu kura milioni 50.5) katika uchaguzi nyeti na muhimu zaidi wa urais wa Brazili katika miongo mitatu iliyopita. Wanasiasa hao wote wawili hawakufanikiwa kupata idadi inayohitajika ya kura ili kushinda duru ya kwanza. Duru ya pili na ngumu ya uchaguzi huo itafanyika mnamo Oktoba 30.

Karibu wapiga kura milioni 165 wa Brazil walikamilisha masharti ya kupiga kura jana Jumapili, wakati kura za maoni zilionyesha kuwa kiongozi wa mrengo wa kushoto wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva, alikuwa akiongoza kwa kishindo dhidi ya rais anayeondoka wa mrengo wa kulia, Jair Bolsonaro.

Kabla ya uchaguzi wa jana, Lula na Bolsonaro walirushiana tuhuma za ufisadi katika mjadala wao wa mwisho, huku Rais Bolsonaro akimtaja mpinzani wake wa mrengo wa kushoto, Luiz Inacio Lula da Silva, kuwa ni mkuu wa genge la wahalifu lililoendesha "serikali ya wezi" kati ya mwaka 2003-2010.

Kwa upande wake, Lula alimtaja Bolsonaro kuwa ni kidhabi "asiye na aibu" ambaye serikali yake ilificha ufisadi katika ununuzi wa chanjo wakati wa janga la "Covid-19", ambalo liligharimu maisha ya zaidi ya Wabrazili 680,000.

Tags