Oct 22, 2022 02:40 UTC
  • Kufichuliwa kashfa ya ujasusi wa utawala wa Kizayuni nchini Malaysia

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Malaysia, Hamzah bin Zainudin, ametangaza kuwa nchi hiyo imeanza uchunguzi kuhusu nafasi ya shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (MOSSAD) katika kutekwa nyara Mpalestina huko Kuala Lumpur.

Vyombo vya habari vya Malaysia vilmeripoti kuwa genge kubwa la kijasusi la Mossad limesambaratishwa nchini humo. Ripoti zinasema, shirika la ujasusi la Israel limewaajiri zaidi ya Wamalaysia kumi na limekuwa likiwajasisi Wapalestina wanaoishi Malaysia na kuwateka nyara. Mpalestina huyo aliyetekwa nyara na maajenti wa Mossad alikombolewa katika operesheni ya polisi wa Malaysia, lakini vyombo vya habari na duru za usalama zinatahadharisha kuhusu ujasusi wa Mossad. 

Katika miezi ya hivi karibuni, kumetolewa ripoti nyingi katika vyombo vya habari duniani kuhusu ujasusi wa mashirika ya kijasusi na makampuni yanayozalisha programu hatari na mbaya ya utawala wa Kizayuni, jambo ambalo limezua wasiwasi mkubwa kimataifa. Miongoni mwa makampuni hayo ni pamoja na kampuni ya Kizayuni ya Candiru inayojishughulisha na ujasusi, na kampuni ya programu za ujasusi ya NSO ambayo hivi karibuni kulifichuliwa kuwa ilidukua na kufanya ujasusi katika nchi mbalimbali kama vile Lebanon na Uhispania. Wanasiasa mashuhuri kimataifa kama Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Charles Michel, Rais wa sasa wa Baraza la Ulaya ni miongoni mwa wahanga wa programu hiyo ya ujasusi ya Israel. 

Yahya Dabouq, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: “Iwapo nchi mbalimbali hususan za Kiislamu hazitachukua hatua kali dhidi ya maajenti wa mashirika ya kijasusi ya Kizayuni, jambo hilo litakuwa na matokeo hatari sana. Kwa sababu utawala huu, ambao unakabiliwa na chuki ya kimataifa, hauna njia nyingine ila kutumia zana za kijasusi, ambazo hivi karibuni ziliuibulia kashfa kubwa." 

Moja kati ya nchi muhimu za Kiislamu ambazo ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ni Malaysia. Licha ya juhudi kubwa za Wazayuni za kutaka kuanzisha uhusiano na nchi za Kiislamu kwa kutumbia mbinu tofauti, Malaysia ingali inapinga uwepo wa utawala huo wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina na inalaani uhusiano wa aina yoyote na Israel na kuwaunga mkono Wapalestina na mapambano yao ya ukombozi. Katika hali hiyo, Wapalestina wana nafasi nzuri nchini Malaysia, na jambo hili linawakasirisha mno Wazayuni. Kwa msingi huo, utawala wa Kizayuni unatekeleza sehemu muhimu ya mipango yake ya kijasusi nchini Malaysia na unajaribu kupata taarifa na mipango ya Wapalestina dhidi ya utawala wa huo haramu kwa kuwateka nyara Wapalestina. Aghalabu ya Wapalestina wanaoishi Malaysia wameelimika na wanahesabiwa kuwa miongoni mwa wasomi wanaotambuliwa na Israel kuwa vinara wa harakati na wanamapambano wa Kipalestina.

Nasser Qandil, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema: "Wapalestina katika nchi zote za Kiislamu wanatumia suhula za nchi hizo kuimarisha misimamo yao, na kwa sababu hiyo utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa kukabiliana na makundi ya Palestina hadi hivi sasa."

Kwa vyovyote vile, suala la uwepo na ushawishi wa Wazayuni nchini Malaysia si jambo dogo na rahisi, na kwa sababu hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Malaysia ametangaza kuanza uchunguzi wa kina kuhusiana na kadhia hiyo.

Kuwepo majasusi wa Mossad Kusini Mashariki mwa Asia ni kengele ya hatari kwa nchi za eneo hilo

Suala linalotia wasiwasi zaidi ni kuona Wazayuni wakitumia kiwango kikubwa cha fedha kuwaajiri raia wa Malaysia kama majasusi, na hapana shaka kuwa, kutokabiliana na suala hjilo yumkini kukapelekea kuundwa mtandao mkubwa na mpana zaidi wa Mossad nchini humo na kuifanya Malaysia kituo kikuu cha ujasusi wa Mossad katika eneo hilo la Kusini Mashariki mwa Asia. Hadi sasa Wazayuni hawajafanikiwa kuwa na nafasi muhimu katika eneo hilo la Asia. Kwa sababu hiyo shirika la ujasusi la Mossad la utawala wa Kizayuni linafanya kazi kubwa zaidi katika eneo hilo, na hivi karibuni pia kulifichuliwa ujasusi wa shirika hilo dhidi ya maafisa wa serikali ya Indonesia.

Kwa hivyo, kufichuliwa ujasusi wa Mossad nchini Malaysia kunapiga kengele ya hatari kuhusu uwepo wa majasusi wa Kizayuni katika eneo la Kusini Mashariki mwa Asia, suala ambalo linapaswa kupewa umuhimu si na serikali ya Kuala Lumpur pekee, bali pia nchi nyingine za eneo hilo ikiwemo Indonesia.  

Tags