Nov 28, 2022 06:53 UTC
  • NATO: Ulaya inakabiliwa na 'wakati mgumu' kwa kuipa himaya Ukraine

Katibu Mkuu wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) amekiri kuwa, kuiunga mkono Ukraine katika vita dhidi ya Russia kumezipelekea nchi za Ulaya kukumbwa na matatizo mengi ukiwemo mfumko wa bei.

Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa NATO ameliambia gazeti la Ujerumani la Welt an Sonntag kuwa, ingawaje kuiunga mkono Ukraine kunawafanya wananchi wa Ulaya wakabiliwe na changamoto tele, lakini anasisitiza kuwa nchi wanachama wa NATO na waitifaki wao hawana budi kuendelea kuizatiti Ukraine kwa silaha na zana za kivita.

Amesema, "Ongezeko la bei za chakula na nishati linamaanisha 'wakati mgumu' kwa familia nyingi barani Ulaya. Hata hivyo walioathiriwa wanapaswa kufahamu kuwa, wananchi wa Ukraine ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi kwa kutoa muhanga damu zao kila siku."

Katibu Mkuu wa NATO sanjari na kuipongeza Ujerumani kwa kuipa Ukraine silaha amedai kuwa, "Magharibi inaweza kuimarisha nafasi ya Ukraine katika meza ya mazungumzo, iwapo tutaipa nchi hiyo uungaji mkono wa kijeshi. Njia bora zaidi ya kuunga mkono amani ni kuisaidia (kijeshi) Ukraine."

Silaha za Wamagharibi zikiwasili Ukraine

Hii ni katika hali ambayo, jarida la Economist limeonya kuwa, kuna uwezekano wa kutokea vifo 147,000 katika msimu wa baridi kali huko Ulaya kwa kuzingatia gharama za sasa za kupanda kwa bei ya nishati. Aidha iwapo baridi itaongezeka na kuwa kali zaidi idadi ya vifo itafikia 185,000 katika nchi za Ulaya. 

Mgogoro wa nishati uliosababishwa na nchi za Ulaya kuiwekea vikwazo Russia umezidi kuwa mkubwa, hususan katika msimu huu wa baridi kali.

Tags