UN yaunga mkono kutambuliwa Siku ya Nakba ya Wapalestina
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuunga mkono azimio lenye maslahi kwa Palestina la kutaka kuadhimishwa Siku ya Nakba, inayokumbusha tukio chungu la kuasisiwa utawala bandia na haramu wa Israel mwaka 1948.
Azimio hilo limepasishwa kwa kura 90 za 'Ndio' na 30 za 'Hapana.' Nchi 47 zimejizuia kuipigia kura rasimu ya azimio hilo. Azimio hilo limepasishwa licha ya pingamizi la Marekani, Israel, na Uingereza. Nchi nyingine zilizopinga azimio hilo ni Australia, Austria, Canada, Denmark, Ujerumani, Ugiriki, Hungary, Italia, na Uholanzi.
Rasimu ya azimio hilo iliyopasishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilidhaminiwa na Misri, Tunisia, Jordan, Senegal, Yemen na Wapalestina.
Azimio hilo la Baraza Kuu la UN limetoa mwito wa kuadhimishwa mwaka wa 75 wa Siku ya Nakba mnamo Mei mwaka ujao 2023 katika ukumbi wa taasisi hiyo, sanjari na kusambazwa nyaraka za kumbukizi na ithibati za tukio la Nakba.
Miaka 74 iliyopita, utawala haramu na bandia wa Kizayuni wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya jinai kadhaa za kinyama dhidi ya Wapalestina.

Mei mwaka 1948, zaidi ya robo tatu ya eneo la kihistoria na la asili la ardhi ya Palestina lilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu, Wapalestina 531 waliuliwa; mbali na kufukuzwa na kugeuzwa wakimbizi karibu asilimia 85 ya idadi ya watu wa Palestina waliolazimika kukimbilia nchi jirani ikiwemo Jordan, Syria, Lebanon na baadhi ya nchi nyingine za nje ya Ukanda wa Asia Magharibi.
Katika kipindi hicho cha miongo saba na nusu iliyopita, zaidi ya asilimia 85 ya ardhi ya Palestina imevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Pamoja na hayo, utawala huo ghasibu ungali unaendeleza ujenzi haramu wa vitongoji na ungali una uchu na tamaa ya kupora ardhi na nyumba zaidi za Wapalestina.