Dec 27, 2022 02:28 UTC
  • Kukirihishwa polisi na vyombo vya habari vya Magharibi katika kukabiliana na kuakisi ugaidi wa Wazungu

Shambulio la kigaidi na la ubaguzi wa rangi lililotokea hivi karibuni Paris, mji mkuu wa Ufaransa, kwa mara nyingine limeonesha jinsi polisi na vyombo vya habari vya Magharibi vinavyokirihishwa, kuchukizwa na kutopenda kabisa kukabiliana na kuakisi vitendo vya kigaidi vinavyoifanywa na Wazungu magaidi.

Raia mmoja wa Ufaransa ametiwa mbaroni kwa kuhusika na shambulio la hivi karibuni kwenye eneo lenye Wakurdi wengi mjini Paris. Gaidi huyo ametangaza bila ya kiwewe kuwa amefanya shambulizi hilo kutokana na chuki zake kubwa kwa wageni. Gaidi huyo mwenye umri wa miaka 69, anashikiliwa na polisi wa Ufaransa hivi sasa kwa kufanya shambulio siku ya Ijumaa ya tarehe 23 Disemba, 2022 katika kituo cha utamaduni cha Wakurdi na mkahawa mmoja katika manispaa ya 10 ya Paris. Wanaume wawili na mwanamke mmoja wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.

Gaidi huyo Mzungu ambaye inasemekana ni dereva mstaafu wa treni ambaye pia ana historia mbaya ya kushambulia watu kwa visu, alikuwa hana nyumba ya kuishi bali akipitisha maisha yake kwenye maboksi na kuzurura mitaani. Alikuwa ameachiliwa huru kutoka jela tarehe 12 mwezi huu wa Disemba. Mwaka jana gaidi huyo alishambulia kambi ya wakimbizi kwa chuki na ubaguzi wa kizazi na ingawa shambulizi lake hilo lilistahiki apandishwe kizimbani, lakini sheria haikufuata mkondo wake na hakupandishwa kabisa kizimbani. Badala yake viongozi wa serikali ya Ufaransa waliamua kumwachilia huru na matokeo yake ni kufanya shambulio hili jingine la kigaidi dhidi ya Wakurdi. 

Machafuko Paris baada ya gaidi Mzungu kuua kigaidi wageni watatu mjini Paris

 

Baada ya kutokea shambulio la kigaidi mjini Paris hivi karibuni na kuuliwa kidhulma watu watatu wasio na hatia, hivi sasa kila mtu anashangaa kuona kwa nini vyombo vya habari vya Magharibi vimeamua kutolipa uzito wowote shambulio hilo lililofanywa na Mzungu gaidi na kwa nini polisi wa Ufaransa wanakuwa na kigugumizi cha kukabiliana na gaidi huyo Mzungu? Baya zaidi ni kuwa vyombo vya habari vya Magharibi vinajaribu kulififiliza shambulio hilo la kigaidi kama vinavyoyafifiliza mashambulio yote ya kigaidi yanayofanywa na Wazungu.

Hii ni katika hali ambayo, vyombo hivyo hivyo vya habari vya Magharibi vinaongeza chumvi sana na kukuza kupindukiza tukio lolote baya linalofanywa na wageni hasa wenye majina ya Kiislamu hata kama mtu huyo haheshimu hata chembe mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Polisi wa nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa, pia wanatumia nguvu kupita kiasi kukabilana na matukio kama hayo wakati yanapofanywa na wasio Wazungu hasa wenye majina ya Kiislamu. 

Sayyid Mohsen Abbas, mwandishi na mchambuzi wa kisiasa anayeishi mjini London UIngereza anasema kuhusu undumilakuwili huo wa polisi na vyombo vya habari vya Magharibi kwamba: Kila mtu anajua kuwa shambulio dhidi ya Wakurdi huko Paris ni la kigaidi na la kibaguzi. Lakini taasisi za polisi na za kukabiliana na ugaidi za nchi za Magharibi daima zinakirihishwa na zinachukia kutaja majina na wasifu wa kina wa Wazungu magaidi na wenyeji wa barani Ulaya. Muda wote taasisi hizo zinatumia visingizio vingine kama kudai kuwa magaidi Wazungu ni wendawazimu na wenye matatizo ya kiakili na kisaikolojia. Lakini uhakika ni kuwa, Ulaya na katika nchi zote za Magharibi, kila kona hivi sasa kunashuhudiwa kupata nguvu magenge yenye misimamo mikali ya kulia ambayo yanapenda kufanya ukatili, mauaji na jinai nyinginezo kama hizo.

Polisi wakikandamiza maandamano ya amani mjini Paris ya kulalamikia undumilakuwili wa polisi hao

 

Ukatili unaozidi kuongezeka kutoka kwa magenge yenye misimamo mikali ya kulia barani Ulaya na katika nchi za Magharibi kiujumla, ni jakamoyo kwa wageni hasa Waislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi na hilo liko wazi kabisa na halifichiki. Watu wa mirengo yenye misimamo mikali inazidi kuongezeka na inapata nguvu kwa sera zao za kuchukia sana wageni na kutaka Wazungu tu ndio waishi katika nchi za Magharibi. Ongezeko la fikra hizo potofu lakini ni hatari sana. Hatari yake si kwa wahamiaji tu, lakini pia kwa jamii za Magharibi zenyewe kwani kampeni yao si kitu kingine ghairi ya kuhatarisha tu usalama wa nchi hizo na haitekelezeki kivitendo. Baya zaidi ni kuwa magenge na mirengo hiyo yote inakuwa ni ile yenye chuki na dini tukufu ya Uislamu. 

Ilkka Salmi, mratibu wa vita dhidi ya ugaidi ndani ya Umoja a Ulaya anazungumzia hatari za magenge ya kigaidi na kusema, vitisho kutoka kwa makundi yenye misimamo mikali ya Wazungu hususan yale yanayopenda kufanya mauaji na kutumia nguvu, vimeongezeka sana hivi sasa barani Ulaya.

Tags