China yarekodi vifo karibu 60,000 vinavyohusishwa na COVID-19
China imesema watu karibu 60,000 waliaga dunia kutokana na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha mwezi mmoja, huku nchi hiyo ikakabiliana na wimbi jipya la maambukizi ya ugonjwa huo.
Afisa wa Kamisheni ya Taifa ya Afya ya China (NHC) hapo jana Jumamosi alitangaza kuwa, vifo 59,938 vinavyohusishwa na maradhi ya COVID-19 viliripotiwa nchini humo baina ya Disemba 8 mwaka uliomalizika 2022, na Januari 12 mwaka huu.
Jiao Yahui, Mkuu wa Idara ya Matibabu ya NHC amewaambia waandishi wa habari kuwa, vifo 5,503 vilisababishwa moja kwa moja na matatizo ya kupumua yaliyotokana na virusi vya Corona, huku 54,435 vikitokana na magonjwa sugu yaliyokuwa yakiwasumbua watu waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.
Beijing mwezi uliopita ilisema itajumuisha tu vifo vilivyosababishwa moja kwa moja na ugonjwa wa COVID-19 katika takwimu zak za vifo vya maradhi hayo, hatua ambayo ilikosolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni, serikali ya China ilitangaza kufungua tena mipaka yake kwa wageni wa kimataifa kwa mara ya kwanza tangu ilipoweka vizuizi vya kusafiri mnamo Machi 2020 kufuatia janga la kimataifa la Corona.

Tangazo hilo lilitolewa wakati huu ambapo China inapambana na ongezeko la visa vya maambukizi na vifo vya ugonjwa wa COVID-19; hali ambayo imezua wasiwasi.
Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, kuna matumaini kwamba janga la dunia nzima la Corona litamalizika mwaka huu wa 2023.