Feb 12, 2023 02:34 UTC
  • Onyo la Putin kuhusu kukithiri kwa vitisho vya kigaidi nchini Afghanistan

Rais wa Russia, Vladimir Putin amesema kwamba: "Tishio la ugaidi limeongezeka baada ya Marekani kuondoka Afghanistan."

Putin ameyasema hayo katika Mkutano wa Jukwaa la Usalama wa Eneo unaojadili hali ya kiusalama, kisiasa na kijamii ya Afghanistan ulioanza Jumatano iliyopita huko Moscow. Mkutano huo umehudhuriwa na makatibu wa mabaraza ya usalama, washauri na wawakilishi kutoka nchi za Russia, Iran, India, China, Tajikistan, Kyrgyzstan, Uzbekistan na Turkmenistan. Lengo la mkutano huo ni kuzuia kuenea machafuko ya sasa huko Afghanistan hadi kwenye nchi jirani. Afghanistan ilikumbwa na machafuko na ukosefu wa amani baada ya uvamizi na mashambulizi ya Marekani na waitifaki wake katika nchi hiyo.

Katika muktadha huo, runinga ya Russia Today imemnukuu Rais Vladimir Putin akisema: Russia ina wasiwasi kwamba nchi za nje ya eneo hilo zitatumia hali mbaya ya Afghanistan kwa ajili ya kuanzisha vituo na kambi za kijeshi nchini humo. Tangu Marekani ilipoondoka Afghanistan, tishio la ugaidi ndani ya nchi hiyo limeongezeka. Vilevile kilimo cha dawa za kulevya na shughuli zinazohusiana na ulanguzi wa dawa hizo vinaongezeka nchini Afghanistan.

Hali ya Afghanistan si shwari na harakati za kundi la al-Qaida pia zimeongezeka nchini humo. Ni vyema kutambua kwamba Marekani, ambayo iliishambulia Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kulazimika kuikimbia nchi hiyo kwa fedheha mwezi Agosti 2021 baada ya miaka 20 ya uvamizi usio na tija, bado inadai kupambana na ugaidi katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Kuhusiana na suala hilo, Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, alidai katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa kuondolewa wanajeshi wa nchi yake huko Afghanistan kwamba: "Juhudi za Marekani za kupambana na ugaidi nchini Afghanistan bado zinaendelea".

Marekani iliivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan wakati wa uongozi wa George W. Bush, baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, kwa kisingizio cha kile kilichotajwa ni mapambano ya kimataifa dhidi ya ugaidi na kuiangusha serikali ya Taliban, ambayo iliituhumu kushirikiana na Al. -Qaeda. Katika kilele cha uvamizi huo mnamo 2011, idadi ya askari wa Marekani na NATO katika nchi hiyo ilifikia zaidi ya watu laki moja na 40 elfu. Hata hivyo, kuwepo kwa vikosi vya majeshi ya Marekani na NATO katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita katika kipindi cha miaka 20, hakukuwa na matokeo yoyote chanya isipokuwa kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, umaskini, uzalishaji na biashara ya madawa ya kulevya, na kupanuka zaidi harakati za kigaidi.

Aidha, wakati wa kuikaliwa kwa mabavu Afghanistan, kundi la Taliban ambalo Marekani ilidai kupambana nao lakini lilitia saini makubaliano na kundi hilo wakati wa utawala wa Trump ili ijitoe Afghanistan, lilipata nguvu zaidi na hatimaye kuiteka Kabul Agosti 2021 na kupindua serikali kuu ya Afghanistan. Kundi hilo sasa ndilo linaloongoza Afghanistan. Hata hivyo, matukio hayo ya kisiasa na kijeshi si tu kwamba hayakupelekea kutokomezwa ugaidi nchini Afghanistan, bali mashambulizi ya kigaidi ya kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS) yameongezeka, na wanachama wake wanawaua Waislamu wa madhehebu za Shia na Sunni kwa mashambulizi ya silaha na milipuko ya mabomu.

Suala muhimu ni kwamba mwishoni mwa kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na baada ya kuasisiwa kundi la ISIS nchini humo, Marekani imekuwa ikitoa misaada mingi ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja kwa kundi hilo la kigaidi kwa ajili ya kuibua hali ya ukosefu wa amani katika nchi jirani. Inaonekana kuwa hai hiyo bado inaendelea.

Zamir Kabulov, mwakilishi maalumu wa serikali ya Russia katika masuala ya Afghanistan alitangaza wiki iliyopita kuwa nchi yake ina ushahidi kwamba Marekani inajaribu kuanzisha njia ya mawasiliano na wapinzani wa utawala wa sasa nchini Afghanistan. Kabulov anasema: Ushahidi ambao Russia inao unaonyesha kuwa Marekani inawahami na kuwasaidia kwa siri magaidi wa ISIS na kwamba inafanya hiyo kulipiza kisasi kwa kushindwa kwake kisiasa huko Afghanistan.

Baada ya kuondoka Marekani kwa fedheha nchini Afghanistan mnamo Agosti 2021, wigo wa mashambulio ya kigaidi ya ISIS nchini Afghanistan umeongezeka sana na mamia ya watu wameuawa. Marekani daima imekuwa ikilitumia kundi la Daesh (ISIS) kama chombo dhidi ya maadui zake, hasa Russia na Uchina; na kuimarishwa kundi hilo nchini Afghanistan, haswa katika maeneo ya jirani na nchi za Asia ya Kati kama Tajikistan na Uzbekistan, kunafanyika kwa lengo la kuziwekea mashinikizo Russia na China.

Afghanistan

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa, Pir Mohammad Mollazehi anasema:
“Marekani imejaza nafasi yake tupu nchini Afghanistan kwa kutumia wapiganaji wa Daesh.”

Hali hii inaonyesha waziwazi uongo wa madai ya Wamarekani kuhusu vita dhidi ya ISIS na kubainisha kuwa ISIS kamwe haiwezi kufanya jinai na uhalifu bila ya himaya na uungaji mkono wa Washington.

Tags