Feb 21, 2023 07:21 UTC
  • Baraza la Usalama lalaani ujenzi wa vitongoji haramu Palestina inayokaliwa kwa mabavu

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha rasimu ya azimio linalolaani uamuzi wa serikali ya Israel yenye misimamo ya kufurutu ada ya Benjamin Netanyahu wa kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya tisa katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Taarifa ya Baraza hilo iliyosomwa jana Jumatatu na Vanessa Frazier, Mwakilishi wa Kudumu wa Malta katika Umoja wa Mataifa imesema: Baraza la Usalama linakariri kuwa, kuendeleza ujenzi wa vitongoji kunakofanywa na Israel kunauweka hatarini uwezekano wa kufikia suluhu baina ya Israel na Palestina kwa misingi ya mipaka ya 1967. 

Amesema Baraza la Usalama limetiwa wasiwasi na tangazo la Februari 12 la Israel, kwamba utawala huo utafanya upanuzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Baraza la Usalama limesema tangazo hilo la serikali ya Netanyahu la kuidhinisha ujenzi wa vitongoji vipya tisa katika ardhi za Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, linaweka vizingiti zaidi katika barabara ya kusaka amani ya kudumu na endelevu.

Hatua hii ni pigo jipya kwa njama za serikali mpya ya utawala wa Kizayuni wa Israel yenye misimamo mikali inayoongozwa na Benjamin Netanyahu, za kupora ardhi zaidi za Palestina. 

Ujenzi haramu katika ardhi za Wapalestina zilizoghusubiwa

Baraza la Usalama lilifanya kikao hicho jana, ikiwa ni jibu lake kwa tangazo la karibuni la utawala wa Kizayuni kwamba unapanga kuhalalisha ujenzi wa vituo tisa vya nje na kuendeleza mipango ya kujenga nyumba mpya elfu kumi za walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. 

Azimio hilo kwa mara nyingine tena limethibitisha kwamba, kitendo cha Israel cha kujenga vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1967, ikiwemo Mashariki ya mwa al-Quds, si halali na ni kinyume cha kisheria, na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

 

Tags