Moscow: US inazishinikiza nchi za Afrika zikate uhusiano na Russia
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema nchi za Afrika hivi sasa zinashuhudia mashinikizo makubwa ya kuzitaka zikate uhusiano wao na Russia.
Mikhail Bogdanov amenukuliwa akisema hayo na shirika la habari la TASS na kuongeza kuwa, "Marekani na waitifaki wake wanafanya kampeni kubwa ambayo haijawahi kushuhudiwa ili Russia itengwe kisiasa na kiuchumi."
Mwanadiplomasia huyo wa Russia amesema nchi za Magharibi zilianzisha kampeni kubwa ya kutaka jamii ya kimataifa iitenge Russia baada ya Moscow kuanzisha operesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya Ukraine mnamo Februari mwaka jana 2022.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza bayana kuwa, tangu operesheni hiyo ya kijeshi ianze, nchi za Magharibi zimeshadidisha mashinikizo dhidi ya nchi za Afrika, na kuzitishia kuziwekea vikwazo au kuzikatia misaada ya kifedha na kibinadamu.
Bogdanov amesema sehemu ya kampeni hiyo ya Wamagharibi, ni kujaribu kuvuruga mkutano wa pili wa Russia na Afrika, unaotazamiwa kufanyika mjini St. Petersburg mnamo Julai mwaka huu, kwa uenyeji wa Rais Vladimir Putin.
Awali mwanadiplomasia huyo alibainisha kuwa, kufuatia matokeo ya mkutano wa kwanza wa kilele wa Russia na Afrika uliofanyika Sochi mwaka 2019, maamuzi yalifanywa ambayo ni pamoja na "kupanua uwepo wa kidiplomasia wa Russia barani Afrika."
Bogdanov amesema, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia inafanya jitihada za kufungua balozi mpya katika nchi kadhaa za Afrika.