Russia: US inatuma magaidi Afghanistan kuyumbisha uthabiti wa eneo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i97990-russia_us_inatuma_magaidi_afghanistan_kuyumbisha_uthabiti_wa_eneo
Russia imeituhumu Marekani kuwa inataka kutumia magenge ya kigaidi nchini Afghanistan kwa shabaha ya kuvuruga uthabiti katika eneo zima la Asia ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 26, 2023 09:45 UTC
  • Russia: US inatuma magaidi Afghanistan kuyumbisha uthabiti wa eneo

Russia imeituhumu Marekani kuwa inataka kutumia magenge ya kigaidi nchini Afghanistan kwa shabaha ya kuvuruga uthabiti katika eneo zima la Asia ya Kati.

Shirika la habari la ITAR-TASS limemnukuu Waziri wa Ulinzi wa Russia, Sergei Shoigu akisema hayo na kuongeza kuwa, Afghanistan inasalia kuwa kitovu cha ukosefu wa uthabiti, na kwamba tishio kuu linatokana na kushtadi harakati za magenge haramu yaliyojizatiti kwa silaha nchini humo, tokeo Taliban itwawe madaraka ya nchi.

Shoigu amesema hayo huko Minsk, mji mkuu wa Belarus, katika hotuba yake mbele ya mkutano wa wakuu wa ulinzi wa Shirika Jumuishi la Mkataba wa Usalama (CSTO), ambao ni muungano wa kijeshi wa nchi za eneo la Eurasia.

Waziri wa Ulinzi wa Russia amebainisha kuwa, "Tunaitakidi kuwa Marekani inapania kutumia magenge haya ya kigaidi kuyumbisha hali ya mambo katika eneo."

Magaidi Afghanistan

Ameongeza kuwa, ili kufanikisha mpango huo ghalati, Marekani tayari imeyakusanya magenge ya wapiganaji katika eneo la Asia ya Kati, ili kuyatuma nchini Afghanistan.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikituhumiwa na duru mbalimbali kwamba inakula njama za kujaribu kuigeuza Afghanistan kuwa kimbilio na kitovu cha ugaidi. 

Waziri wa Ulinzi wa Russia anasisitiza kuwa, Marekani inafanya kila iwezalo kuifanya Afghanistan kuwa kituo chake kikuu cha kueneza ugaidi na ukosefu wa usalama katika pembe mbalimbali za kanda ya Mashariki ya Kati.