Jul 14, 2023 11:49 UTC
  • Biden aonya: Kuipatia Ukraine uanachama wa NATO wakati wa vita kutaishia kwenye Vita vya Tatu vya Dunia

Rais Joe Biden wa Marekani ameonya kuwa uwezekano wa Ukraine kujiunga na NATO wakati iko vitani na Russia huenda matokeo yake ya mwisho yakawa ni kuzuka Vita vya Tatu vya Dunia.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari aliofanya mjini Helsinki jana akiwa na Rais Sauli Niinisto wa Finland, Biden alisema, "hakuna mtu anayeweza kujiunga na NATO wakati vita vinaendelea, kwa sababu hiyo itahakikisha kwamba tuko kwenye vita, tuko kwenye Vita vya Tatu vya Dunia".

Rais huyo wa Marekani alisema kuhusu uwezekano wa Ukraine kujiunga na shirika hilo la kijeshi la nchi za Magharibi kwamba, suala "si kuhusu iwapo wanafaa au hawafai kujiunga, ni kuhusu lini wanaweza kujiunga."

Kifungu cha 5 cha mkataba wa NATO kinasema, shambulio dhidi ya mwanachama mmoja ni shambulio dhidi ya wanachama wote, ikiwa na maana kwamba endapo Ukraine itaingizwa kwenye jumuiya hiyo wakati bado iko vitani, wanachama wote wa NATO watapaswa kuingia katika vita kamili na vya moja kwa moja na Russia; na hiyo sio nia ya kambi hiyo ya kijeshi ya Magharibi kwa sasa.

Rais Putin wa Russia (kushoto) na Rais Biden wa Marekani

 

Alipoelezwa kwamba ikiwa Ukraine haiwezi kujiunga na NATO sasa hivi, hatua hiyo itamhamasisha Rais Vladimir Putin wa Russia, Biden alisema, hafikirii kama vita vitaendelea kwa miaka mingi kwa sababu Russia haiwezi kuendelea kubakiwa na suhula na zana zake kwa muda mrefu.

Hayo yanajiri huku maafisa wa Ukraine wakitangaza kuwa wamepokea shehena ya mabomu yenye utata ya vishada (cluster bombs) kutoka Marekani.

Ikulu ya White House ilitangulia kuthibitisha kwamba Marekani itaipatia Ukraine mabomu ya vishada yaliyopigwa marufuku kimataifa kusaidia katika mashambulizi yake dhidi ya vikosi vya Russia.

Mabomu ya vishada yamepigwa marufuku chini ya Mkataba wa Mabomu ya Vishada (CCM), mkataba wa kimataifa ambao unashughulikia athari kwa kibinadamu na madhara yasiyokubalika yanayosababishwa na mabomu hayo kwa raia.../

 

Tags